Sunday, September 16, 2012

HUU NDO UKWELI WA MAISHA YA WASANII WA BONGO MOVIE


WENGI wanaamini kuwa maisha ya wasanii wa filamu ni ya kitajiri na kwamba hawana shida kabisa za maisha, hata hivyo ukweli haupo hivyo kabisa.

Maisha yao yamejaaa changamoto nyingi na linapokuja suala la wasanii kuendeleza mwonekano wao mbele ya umma, huwagharimu mno baadhi ya wasanii kiasi cha wengi wao kuishi maisha ya kufoji.

Mpekuzi  imegundua kuhusu maisha hayo ya kuigiza kwa wasanii wengi ambao ni nyota katika tasnia ya filamu za Swahiliwood.

Mara nyingi wasanii hao wamejikuta wakiingia lawama kutoka kwa baadhi ya ndugu zao baada ya kuombwa misaada kwa kuhisiwa wana uwezo.

Wanaposhindwa kutoa misaada hiyo ndipo wanapoingia matatani.

Hivi karibuni mmoja wa wasanii nyota katika tasnia hiyo aliwaambia wanahabari kuwa wasanii wana maisha mabaya kuliko wanavyofikiriwa.

"Jamani msituone hivi, tuna hali mbaya sana. Maisha yetu yamefikia pabaya kwa sababu ya maharamia wa filamu zetu, tunavyoonekana katika filamu si maisha tunayoishi mitaani," alisema.

"Hatuna hizo fedha wanazofikiria watazamaji wetu, narudia tena maisha yetu mabaya sana."

Wasanii wengi wamekuwa wakiishi kwa maisha ya kuigiza kwa kujaribu kujionesha kuwa wana miliki magari ya kifahari wakati ukweli haupo hivyo, japo wengi wanakataa kusema ukweli.

Maisha hayo yanatokana na wasanii kujaribu kujiweka juu kama walivyo wenzao wa nchi nyingine.

NYUMBA
Inasemekana kuwa wasanii wengi katika tasnia ya filamu za Swahiliwood, wanaishi katika nyumba za kupanga hasa maeneo ya Sinza, Tabata, Mwananyamala na Kijitonyama (kwa Dar es Salaam).

Hata wale wanaoishi katika nyumba za familia ni rahisi kukubali hilo iwapo tu nyumba hizo zipo katika maeneo yenye hadhi.

Lakini ni tofauti na wasanii wanaoigiza vichekesho, kwa mfano wasanii wa Komedi wao wanamiliki nyumba katika sehemu mbalimbali. Masanja, Mac Reagan na Mpoki wao wanamiliki nyumba eneo la Kibada.

Joti anamiliki nyumba yake Ulongoni, Bambo amejenga nyumba Kigogo Mbuyuni, Kingwendu amejenga Mbagala, Mkwere anamiliki nyumba yake Kimara Bonyokwa wakati King Majuto anamiliki nyumba jijini Tanga.

Hawa wote hakuna anayeendesha gari la kifahari hata mmoja, kama yupo basi gari hiyo itakuwa ni Noah.

Pengine linalowafanya wasanii hawa wafanikiwe ni aina ya usanii wao kwani kwao hata daladala wanatumia.

USAFIRI

Katika suala hili, baadhi ya wasanii wamefanikiwa kumiliki magari hata yale ya thamani japo si wote. Lakini wanaonekana kuumia ni akina dada kwani wanalazimka kukodi magari ya gharama kubwa.

Kwa uchunguzi wa Mpekuzi, gharama hizo zinaanzia Sh300,000 kwa gari kama Hammer au Sh250,000 kwa Range Rover, Vogue au Mercdes Benz. Magari kama Toyota Creaster, Nadia, Luxers na Harrier ni Sh150,000 kwa siku.

Kati ya magari hayo, kuna ambayo wasanii hawa hulazimika kuingia mkataba rasmi kwa ajili ya tahadhari, hii ni kwa mujibu wa mmiliki mmoja wa magari.

Mmiliki huyo anasema kinachowaponza wasanii hao ni kutokuwa na moyo wa subira, kwani kila wakishauriwa kuweka fedha ili kununua magari yao, hawashauriki.

"Unajua ni kutokuelewa hesabu. Kama mtu ana uwezo wa kunipatia Sh 3 milioni kwa wiki maana yake ana uwezo wa kununua gari. Tatizo hawa jamaa wanapenda maisha ya kubahatisha," alisema.

"Msanii anaweza pia kwenda kwa wakala wa magari na kukopa lake kisha akawa analipa."


Suala la usafiri ndiyo linalowatesa sana wasanii wa kike na wanapokuwa hawana fedha hukodi teksi zenye vioo vya giza ili wasijulikane.

"Hali inapokuwa ngumu hupanda hata bajaj au boda boda (pikipiki) lakini hujifunika baibui," aliongeza.

Hata kwa wale ambao baadhi yao wamekuwa wakitangaza wanamiliki magari, umiliki huo umejaa utata.

Kuna jamaa mmoja inadaiwa alikuwa anawajazia wasanii hao mafuta kwenye magari yao, lakini baada ya kuyumba kiuchumi hata wasanii hao wameyumba katika suala la usafiri.

MAVAZI.

Kwa upande wa mavazi inasemekana kuwa wasanii wengi hukodi kwa ajili ya kurekodia filamu, lakini kiukweli hawana uwezo wa kumiliki nguo za gharama kubwa.

Msanii pekee ambaye ni bingwa wa mavazi ni Patcho Mwamba ambaye inaamika kuwa hata sababu kubwa ya kuingia katika tasnia hiyo ilikuwa ni baadhi ya wasanii kutumia sana nguo zake kwa maana ya kuazima.

MALIPO

Suala la malipo kwa wasanii bado ni kitendawili kwani hakuna malipo rasmi ambayo yanajulikana kwa ajili ya washiriki wa filamu, malipo hutegemea hisani.

Wasanii waliowahi kulipwa vizuri ni Steven Kanumba (marehemu sasa) katika filamu ya Leither Poison, Hamis Kinzasa "Twenty Percent" katika filamu ya Furaha Iko Wapi.

MONALISA

Yvonne Cherryl 'Monalisa' anasema kuwa hakuna sababu ya kuficha hali halisi ya maisha kwani kwa kufanya hivyo msanii anaweza kukosa watu wa kumsaidia.

"Ni kweli watu wanafoji maisha yao, hawapendi kuonyesha ukweli kuhusu maisha, lakini hilo halipo kwa wasanii wa filamu tu, watu wengi wana tabia hiyo," anasema Monalisa.


ISSA MUSSA
"Sisi wasanii wengi ni waoga wa maisha, tunaigiza hata katika maisha yetu halisi, wasanii wanaosema uongo katika jamii wanafanya hivyo kwa sababu ya kutojipanga na kujaribu kulinda hadhi yao," anasema.

HUSNA POSHI

"Wengi wa wasanii hawana hesabu nzuri za maisha, kuna wanaokodi magari na kusema kuwa ni yao, wanatumia gharama kubwa bila sababu, wanawake hawashauriki na ukimwambia anahisi unamwonea wivu, tunawaacha waishi maisha ya kufoji," alisema msanii huyo anayejulikana kwa jina la Dotnata.

Wasanii hao pia wana sehemu zao wanazopendelea kukutana na kupanga mipango yao, zaidi hukutana Leaders Club, Kinondoni.

Kwa sasa inasemekana kuwa baadhi ya wafanyabiashara kwa upande wa burudani wanawatumia sana wasanii wa filamu katika matamasha mbalimbali kama ni sehemu ya kivutio na si kwa ajili ya kuwawezesha kwa ajili ya kutengeneza fedha.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )