Friday, March 25, 2016

Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange Ampongeza Dr Shein Kwa Ushindi

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, amemtumia salamu za pongezi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa tena na wananchi wa Zanzibar kushika wadhifa huo kwa muhula wa pili cha madaraka.

Salamu hizo zilizotumwa na Jenerali Mwamunyange kwa niaba ya Maofisa, Askari na Watumishi wa Umma wanaofanya kazi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), zilieleza kuwa ushindi wa kishindo wa Dk Shein alioupata unadhihirisha kuwa wananchi wa Zanzibar wameridhishwa na uongozi wake makini na mahiri aliouonesha katika muhula wake wa kwanza wa uongozi wake.

Salamu hizo ziliendelea kueleza kuwa historia ya Dk Shein ya uaminifu, maadili mema na uzalendo aliouonesha katika utumishi wake wa muda mrefu katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika kabla hajawa Rais wa Zanzibar imewapa wananchi imani kubwa kuhusu uongozi wake.

“Mheshimiwa Rais, hapana shaka kuwa katika muhula huu wa pili wa uongozi wako, Zanzibar itashuhudia mafanikio makubwa zaidi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, sambamba na kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu kwa wananchi wote,” ilieleza sehemu ya salamu hizo.

Aidha, salamu hizo za pongezi zilieleza kuwa JWTZ inamhakikishia Dk Shein kuwa itaendelea na utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kwake kama ilivyo desturi ya majeshi nchini. W

akati huo huo, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Zanzibar, Abood Jumbe Mwinyi, naye amemtumia salamu za pongezi Dk Shein kwa ushindi wa kishindo alioupata katika marudio ya uchaguzi wa Zanzibar.

Kwa niaba yake na familia ya Mzee Jumbe, salamu hizo zilitoa pongezi kwa Dk Shein pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ushindi huo na kueleza furaha yake ya moyoni mwake kwa kuona jinsi alivyokiwakilisha chama cha CCM na kukipatia ushindi ambao ulitegemewa.

Nao uongozi na wanachama wa ‘Veteran Young Pioneer Association Zanzibar’ umetoa salamu za pongezi kwa Dk Shein kutokana na ushindi wa kishindo alioupata wa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4 katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio uliofanyika hivi karibuni.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )