Sunday, March 20, 2016

TCRA Yazifunga Kurasa FEKI za Mke wa Rais Janet Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezifungia kurasa za facebook na tovuti ya www.focusvikoba.wapka.mobi baada ya kugundua kuwa zinatumia majina ya viongozi kutapeli watu.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, matapeli wanaofanya uhalifu huo wametumia majina ya Janet Magufuli, ambaye ni mke wa Rais na Samia Suluhu ambaye ni Makamu wa Rais kufanikisha utapeli wao.

Dk Simba alisema mamlaka yake imegundua kuwa wahalifu hao wa mtandao huanzisha tovuti, kurasa za facebook na blogu kwa kutumia majina ya viongozi wakuu wa nchi ili kujipatia fedha kutokana na umaarufu wa watu hao.

Alisema matapeli hao hutumia mitandao hiyo kuwadanganya wananchi kuwa kuna fursa za kupata mikopo au misaada kupitia vikundi vya kusaidiana, maarufu kwa jina la vikoba.

“Kwa mfano kuna matapeli walioanzisha ukurasa wa mtandao wa kijamii wa facebook kwa jina la mke wa Rais, Mama Janet Magufuli na kwa jina ma Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakilenga kujipatia kujipatia fedha,” alisema Dk Simba.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, mtu yeyote haruhusiwi kujitambulisha kwenye mitandao kwa kutumia utambulisho wa mtu mwingine.

Alisema adhabu ya kosa hilo imeainishwa kwenye kifungu cha 15(2) kinachosema anayepatikana na hatia anaweza kutozwa faini isiyopungua Sh5 milioni au mara tatu ya thamani ya kile atakachokuwa amekipata kupitia utapeli.

Aliwataka wananchi kuwa macho dhidi ya mitandao ya kijamii, tovuti na blogu ambazo zinawataka kutuma fedha au kuchangia kitu chochote ili wapewe mikopo au misaada.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )