Monday, March 21, 2016

Waziri Mkuu Atoboa Siri za Mwanajeshi Kuteuliwa Kuongoza Mkoa wa Kagera


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoboa siri ya kuteuliwa mwanajeshi kuongoza Mkoa wa Kagera, moja ya mikoa iliyoko pembezoni na yenye tishio kubwa la wahamiaji haramu na matatizo ya ardhi.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa 26 ya Tanzania Bara na kumteua Meja Jenerali mstaafu, Salum Mustafa Kijuu kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Kagera.

Mbali ya Meja Jenerali mstaafu Kijuu, Rais Magufuli pia aliwateua wanajeshi wengine watatu kuongoza mikoa ya Katavi, Geita na Kigoma katika uteuzi huo wa Machi 13. 

Hao ni Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyunga (Geita), Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga (Katavi) na Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga (Kigoma).

Akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera wiki iliyopita, Waziri Mkuu Majaliwa alisema: “Hapa kwenu Kagera kuna tatizo kubwa la waharamiaji haramu na uvamizi wa ardhi.

"Wavamizi wengine wanalima bangi katika maeneo yetu badala ya kufuga na kulima.

 “Waondoeni au punguzeni maeneo yao na lindeni mipaka yetu. Mapori ya Kimisi na Burigi yamegeuzwa maficho ya wahamiaji haramu,” alieleza Waziri Mkuu.

“Ndio maana tumemleta Meja Jenerali Kijuu. Shughuli yake huyu siyo nyepesi. Atatembea mwenyewe huko. Huyu si alikuwa Kamandi ya Infantry (askari wa miguu), kwa hiyo ataimudu shughuli hii vizuri.”

Mkoa huo umewahi pia kuongozwa na wakuu wa mikoa ambao ni wanajeshi katika miaka ya nyuma na baadhi yao ni Abdallah Twalipo, Tumainieli Kiwelu, Ayoub Simba, Fabian Massawe, Silas Mayunga na Enos Mfuru.

Mkoa wa Kagera unakabiliwa na tishio kubwa la wahamiaji haramu wanaingia nchini kutoka nchi jirani na wanamiliki ardhi kinyume cha sheria kutokana na udhaifu wa viongozi waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia.

Unapakana na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Aidha, Waziri Mkuu aliiagiza Idara ya Uhamiaji nchini hasa mkoani Kagera kubadilika ambapo alihoji kwa nini hawavai sare za jeshi lao na kuingia msituni kusaka wahamiaji haramu badala yake wanavaa suti maofisini.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )