Saturday, April 30, 2016

DPP Amng’ang’ania Zombe na Wenzake Wanne, Awachomoa Watano Baada ya Kubaini Ushahidi Alionao Hauwagusi

Mahakama ya Rufani jana ilianza kusikiliza rufaa dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na askari wenzake wanane kuhusu kesi ya mauaji waliyoshinda.

Katika kesi hiyo namba 358 ya mwaka 2013, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anapinga Zombe na wenzake kuachiwa huru na Mahakama Kuu katika kesi ya mauaji ya watu wanne iliyokuwa ikiwakabili.

Zombe na maofisa wenzake walifunguliwa mashtaka katika Mahakama Kuu wakidaiwa kuwaua watu wanne wakiwamo wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro, Januari 14, 2006.

Mauaji hayo yalifanyika katika msitu wa Mabwepande, Dar es Salaam na waliouawa walikuwa Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo pamoja na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na dereva teksi, Juma Ndugu wa Manzese.

Mahakama Kuu katika hukumu yake ya Agosti 17, 2009 iliwaachia huru washtakiwa wote baada ya kuwaona hawana hatia.

DPP hakuridhika na hukumu hiyo na mwaka huohuo, alikata rufaa Mahakama ya Rufani akidai jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao, na kwamba kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira wa kutosha kuwatia hatiani washtakiwa wote.

Rufaa hiyo pia ilitupiliwa ambali na Mahakama Mei 8, 2013 kutokana na dosari za kisheria zilizobainika kwenye rufaa hiyo.

Baadaye DPP alipeleka maombi Mahakama Kuu aruhusiwe kukata tena rufaa hiyo nje ya muda, ombi ambalo lilikubaliwa.

Hata hivyo, katika shauri hili jipya DPP amewaondoa wajibu rufani watano baada ya kubaini kuwa ushahidi alionao hauwagusi katika rufaa hiyo. 

Waliosalia pamoja na Zombe ni Christopher Bageni, Ahmed Makelle na Rajabu Bakari lakini walioondolewa ni Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Abineth Salo na Festus Gwabisabi.

Katika rufaa hiyo iliyosikilizwa jana na majaji Bernard Luanda, Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage, DPP anapinga hukumu iliyowaachia huru.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Wakili wa Serikali, Timon Vitalis aliieleza Mahakama kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani wajibu rufani hao kwani unadhihirisha walikuwa na nia moja ya kutenda kosa pamoja na mtenda kosa halisi (Koplo Saad Alawi aliyetoroka).

Alisema kuwa kitendo cha wajibu rufani hao ambao ni maofisa wa polisi wenye wajibu na uwezo wa kuzuia uhalifu kuwapo eneo la tukio la mauaji wakashuhudia na kushindwa kuzuia ni dhahiri kuwa walikuwa na nia moja na mtenda kosa.

Kuhusu Zombe, Vitalis alisema kitendo cha kuwaelekeza watuhumiwa namna ya kueleza (walipoitwa kuhojiwa kwenye Tume ya Rais) na kutangaza kuwa watu waliouawa waliuawa kwenye mapambano na polisi ni dhahiri alikuwa akimsaidia mtenda kosa kusema uongo ili kumlinda.

Wakijibu hoja hizo kwa nyakati tofauti, mawakili wa utetezi walisema hakuna ushahidi wa dhahiri wa kuwatia hatiani wajibu rufani hao na kwamba Mahakama Kuu ilitathmini vema na kujiridhisha kuwa hawana hatia.

Hivyo waliiomba Mahakama hiyo iwaone kuwa hawana hatia kwa mashtaka yanayowakabili, huku Wakili Dennis Msafiri akisisitiza kuwa Jamhuri inapaswa kutumia nguvu nyingi kumtafuta muuaji halisi kama walivyoelekezwa na Mahakama Kuu na si kutumia muda mwingi kuendelea kuwang’ang’ania wajibu rufaa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Luanda aliahirisha shauri hilo akisema kuwa wanakwenda kutafakari hoja za pande zote na kwamba wanahitaji muda kuandika uamuzi ambao watautoa pale utakapokuwa tayari.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )