Saturday, April 2, 2016

IPTL Yakanusha Tuhuma Za Rushwa Na Taarifa Za Uongo Zilizochapishwa Na Gazeti La Mwanahalisi


1.Makampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan Africa Power Solutions (T) Limited (PAP), tumesononeshwa sana na taarifa iliyochapishwa na gazeti la kila wiki la MwanaHALISI katika toleo namba 332 la tarehe 28 Machi 2016 lenye kichwa cha habari, “Siri za Kikwete, IPTL zafichuka ”; iliyoambatana na nukuu katika ukurasa wake wa mbele inayosomeka “…hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga alitembeza mlungula.”

2.Taarifa hiyo iliyojaa uongo pamoja na kashfa nzito ya rushwa kwa IPTL/PAP na kwa viongozi waandamizi wa serikali ya awamu ya nne na wengine ambao bado wamo katika serikali hii ya awamu ya tano, imediriki kudai kwa kunukuu maneno yafuatayo,….. “Sethi alitoa rushwa kila mahali, ikiwamo Ikulu, ili kufanikisha mpango wake huo….Alihonga kila mtu. Alitoa rushwa kwa kila aliyeona faili la Escrow. Hadi maofisa wa Ikulu na viongozi waandamizi kutoka wizara ya fedha……..hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga alitembeza mlungula. Ni BoT pekee, ambako hakuhonga au kuombwa rushwa.”

3.Tungependa kukanusha taarifa hizi za shutuma ya rushwa ambazo ni za uongo na uzushi mtupu wenye lengo la kuichafua IPTL na wamiliki wake akiwemo Mwenyekiti Mtendaji, Bw. Harbinder Singh Sethi. Taarifa hizi zisizo na chembe ya ukweli ndani yake zinalenga kuchafua sifa ya Ikulu ambayo ni taasisi nyeti hapa nchini kwa kuihusisha na upokeaji rushwa ambayo ni kosa la jinai kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu.

4.Isitoshe taarifa hizi zimejaa habari za uongo zilizobuniwa kwa nia na madhumuni maovu ya kuichafua sifa za kampuni za IPTL/PAP na mwenyekiti wake Bw. Harbinder Singh Sethi pamoja na kuwachonganisha dhidi ya wananchi wa Tanzania kwa kuwahadaa na kuwaaminisha Watanzania kuwa IPTL/PAP inaendeshwa kwa misingi ya rushwa na udanganyifu, hivyo basi haistahili kufanya biashara hapa nchini.

5.Awali ya yote, tungependa kuutarifu umma wa Watanzania kwamba tuhuma za rushwa ni tuhuma nzito na wala siyo za kunyamaziwa kabisa. Rushwa ni moja kati ya makosa makubwa ya kijinai ambayo vyombo vya dola vinatilia maanani sana. Hivyo basi, kampuni ya IPTL/PAP haiwezi kukaa kimya wakati tuhuma kama hizi zikiendelea kuchapishwa dhidi yake, huku ikiwahusisha viongozi waandamizi wa serikali, bila ya gazeti husika pamoja na mwandishi wa taarifa hizo kutoa udhibitisho wowote wa tuhuma hizo.

6.IPTL/PAP tunaamini kwamba taratibu zote za kukabidhiwa kampuni ya IPTL (ikiwemo mali na madeni halali) zilifuatwa. Tunaamini katika utawala wa sheria ambayo inazingatia haki za kila mtu. Hivyo basi, haitakuwa busara kuendelea kunyamazia vitendo vya kiovu vya kuichafua kampuni yetu vinavyofanywa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kisingizio cha “uhuru wa kutoa maoni” au “uhuru wa vyombo vya habari”. Kama vyombo vya habari walivyo na uhuru wao, vivyo hivyo IPTL/PAP kama kampuni ina uhuru wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria za nchi bila ya kubughudhiwa. Kwa kutuhumu IPTL/PAP au viongozi wake kutoa rushwa, bila kuthibitisha, ni kuihujumu kampuni ili isiweze kutekeleza majukumu yake ya kuchangia ukuwaji wa uchumi wa nchi yetu.

7.Mbali na tuhuma za rushwa, takriban taarifa nzima ya gazeti hilo la MwanaHALISI imejaa uongo uliokubuhu na uzushi usiokuwa na chembe ya aibu. Sehemu ya taarifa hiyo ya gazeti la MwanaHALISI inadai na kunukuliwa “Kampuni hiyo binafsi ilidai kuwa gharama za umeme zilikua asilimia 22.3; na gharama za mtaji asilimia 30 zilikuwa dola za Marekani 38.16 milioni. Hata hivyo, Mahakama ilithibitisha kuwa gharama halisi za mtaji wa IPTL zilikuwa chini ya dola za Marekani 1,000”. Tunapenda kuwataarifu Watanzania kuwa hakuna mahakama yoyote duniani iliyothibitisha madai haya na hii ndiyo sababu kuu ya mwandhishi wa taarifa hii kashindwa kutaja ni mahakama ipi hiyo iliyothibitisha hayo yanayodaiwa na kunukuliwa.

8.Sehemu ya taarifa ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa “Lakini fedha hizo zilichotwa kabla mgogoro huo haujapatiwa ufumbuzi na katika mazingira ya udaganyifu; na kwa kutumia baadhi ya nyaraka ambazo ziligundulika kuwa ni za kugushi… Hata hivyo Sethi alishindwa kuweka uthibitisho wowote kuwa kampuni hiyo inamiliki hisa za kampuni ya Mechmar Limited ya Malaysia ndani ya IPTL.”

Kwa yeyote aliyesoma Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) iliyojulikana kama “Taarifa ya Ukaguzi Maalum Kuhusiana na Miamala Iliyofanyika katika Akaunti ya “Escrow” ya Tegeta, Pamoja na Umiliki wa Kampuni ya IPTL”, anaweza kutambua kuwa tuhuma na madai yaliyonukuliwa hapo juu ni uongo mtupu. Ripoti hiyo ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika ukurasa wake 23 inaeleza kuwa Bw. Harbinder Singh Sethi aliwasilisha “Deed of Assignment of Shares” na Mkataba wa Kuuza na Kununua hisa kati ya PAP na PiperLink Investment kutokana na agizo la kuwasilisha ushahidi wa kununua asilimia 70 za hisa za Mechmar katika IPTL. Si Mkaguzi Mkuu wa Serikali wala chombo chochote cha serikali kilichopata kuthibitisha kuwa nyaraka zilizowasilishwa na Bw. Harbinder Singh Sethi zilikuwa ni za kughushi kama taarifa ya gazeti la MwanaHALISI ilnavyodai na kunukuliwa hapo juu.

9.Sehemu ya taarifa ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa “Malipo hayo kwa PAP yalifanyika bila Waziri wa Nishati, Prof. Sospeter Muhongo, wala BoT kuhakiki uhamishaji wa hisa kutoka Mechmar kwenda PAP; bila PAP kusajili hisa zake nchini; bila PAP kuthibitisha kujisajili Kituo ch Uwekezaji nchini (TIC); na bila kuwa na hati ya mlipa kodi (TIN).” Hizi nazo ni taarifa za uongo zisizokuwa na chembe ya ukweli. Mwandishi amejaribu kutumia mseto wa hoja zisizokuwa na mshiko ili mradi anajenga taswira kuonyesha malipo yaliyofanywa kwa PAP yalikuwa ni malipo ya ubabaishaji.

10.Sehemu ya taarifa hiyo ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa “Serikali ililazimika kukopa “kwa siri” kiasi hicho cha fedha kutoka Stanbic kwa kuweka dhamana ya hati fungani, ili kufanikisha upatikanajiwa fedha za kumlipa Singasinga wa IPTL,” ameeleza mmoja wa maofisa wa Stanbic ambaye ametoka katika benki hiyo hivi karibuni. […] Kigogo huyo anasema, “kwa vile wakubwa walishapanga kumlipa Sethi, kabla ya Desemba 2013, ikabidi wakope benki kwa kuweka dhamana hati fungani zilizoshushwa bei (discounted treasury bills).”

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (iliyotajwa hapo juu) kwenye ukurasa wake wa 16 inaelezea wazi kabisa kuwa umiliki wa hati fungani zilizowekezwa na BoT kutokana na fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta, ulihamishwa kwenda kwa PAP tarehe 6 Desemba, 2013. Madai ya kuwa serikali ilikopa kwa kuweka hati fungani zilizoshushwa bei ni uongo na uzushi usiokuwa na ukweli wowote.

11.Sehemu ya taarifa hiyo ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa “Taarifa zinasema, katika kiasi hicho cha dola 180 milioni, dola takriban 100 milioni, kilitoroshewa nje katika nchi za Falme za Kiarabu, huko Dubai na Afrika Kusini, kabla ya kuhamishiwa tena nchini Austria. Nchini Austria, taarifa zinasema, ndiko ambako mtoto wa mmoja wa waliokuwa viongozi wa juu serikalini, amefungua akaunti.” Hizi ni taarifa za uongo zisizokuwa na chembe ya ukweli na ni tuhuma zisizokuwa na ushahidi wowote.

12.Kwa machache haya ya uongo na uzushi tuliyoyanukuu na mengine mengi ambayo tumeamua kutokuyatolea ufafanuzi kwa nia ya kuiweka taarifa hii kwa ufupi, tungependa kuomba vyombo husika kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na uenezi wa taarifa hizi za kizushi kwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola na kuwahoji ili ukweli wa tuhuma ujulikane. Tunaamini kwamba tabia ya kuikashifu kampuni yetu na kuwakashifu viongozi wa serikali bila ya kuwa na uthibitisho isipokomeshwa, basi nchi itajaa waropokaji na heshima ya serikali na vyombo vyake itaporomoka. Tabia hii isipokomeshwa itaathiri hali ya uwekezaji nchini kwani itawakatisha tamaa wawekezaji wengine wanaotaka kuwekeza nchini.

13.Kwa muhtasari, taarifa zilichochapishwa kwenye makala husika ni uzushi usiokuwa na ukweli wowote. Tungewaomba Watanzania na wote waliosoma au watakaosoma makala husika wazipuuzie taarifa hizo. Pia tunawataka wahariri na wachapishaji wa gazeti la MwanaHALISI kuomba radhi kwa taarifa hizo za kizushi ndani ya siku kumi na nne (14). Kushindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kulifikisha gazeti, wahariri na wachapishaji wake mahakamani.

14.IPTL/PAP tuko tayari kutoa ushirikiano kwa mtu yeyote mwenye ushahidi wa rushwa kufikisha mbele ya vyombo husika na kuhakikisha rushwa inakomeshwa.

15.Tunaomba pia vyombo mbalimbali vinavyohusika na kulinda amani na utengamano wa nchi yetu ikiwemo jeshi la polisi kuwachukulia hatua mwandishi wa makala hiyo na wahariri wa gazeti la MwanaHALISI kwa kuvunja sheria za nchi kwa kuandika habari za uchochezi.
Ahsanteni sana.

Joseph O. R. Makandege (ADVOCATE)
(Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria)
KAIMU MWENYEKITI MTENDAJI
Independent Power Tanzania Limited / Pan African Power Solutions (T) Limited.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )