Tuesday, April 12, 2016

Mke wa Waziri Mkuu atoa msaada wa mashuka kwa akinamama waliojifungua katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa


Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na kutoa msaada wa mashuka kwa akinamama waliojifungua.

Pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Ruangwa kutokana na kuwahudumia vizuri wananchi na kuwaomba  waendelee kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.

Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo jana  wakati alipotembelea wodi ya akinamama waliotoka kujifungua na kufurahishwa na hali ya utoaji huduma hospitalini hapo, ambapo  aliwasisitiza kuendelea moyo huo kwa sababu wao ndio wamebeba dhamana ya afya za wananchi.

“Nimefurahi kukuta wazazi wanahudumiwa vizuri na wenyewe wamekiri kwamba huduma zinazotolewa hospitalini hapa ni za kuridhisha, tofauti na tulivyozoea kusikia wagonjwa wakiwalalamikia wauguzi, hivyo ni jambo la kujivunia, hongereni sana” amesema.

Mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo Hamisa Rashid ambaye amelazwa katika wodi hiyo  amesema alifikishwa hospitalini hapo wiki mbili zilizopita akiwa katika hali mbaya na ameweza kuhudumiwa vizuri na sasa anakaribia kutoka.

“Mimi nilikuwa sijitambui, siwezi kufanya kitu chochote lakini baada ya kuletwa hospitalini hapa madaktari kwa kushirikiana na wauguzi wamenihudumia vizuri na sasa naweza hata kwenda chooni mwenyewe na bila msaada wao mimi ningekuwa nimepoteza maisha kutokana na hali yangu ilivyokuwa,” amesema Hamisa.

Mbali na kutoa msaada huo wa mashuka pia ametoa baiskeli mbili kwa ajili ya wanawake wawili walemavu lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya shughuli zao za kijamii kwa urahisi.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Rehema Omary amemshukuru mke wa Waziri Mkuu kwa msaada huo, ambapo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa awawezeshe kwenda kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na walemavu ikiwemo michezo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji kazi wa mazoea kwa sababu umepitwa na wakati.

Pia amesema amefurahishwa  na kitendo cha wagonjwa kukiri kuwa wanahudumiwa vizuri tofauti na hospitali zingine hivyo kuwataka kuendelea na ari hiyo ya kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )