Friday, April 22, 2016

Rais Magufuli Atema Cheche Kuhusu Mafisadi Wanaolalamika Kutumbuliwa Hadharani

Rais John Magufuli jana aliamua kuwatolea uvivu wadau waliopinga kitendo chake cha kutumia hadhara kumsimamisha kazi mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe.

Rais alimsimamisha kazi Kabwe baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumchongea mtendaji huyo wa jiji kuwa alisaini mikataba miwili ya huduma za usafiri na kusababisha jiji lipoteze mabilioni ya fedha.

Baada ya kusikilia maelezo hayo ya Makonda, Rais Magufuli aliuliza wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere kuwa achukue uamuzi gani na kujibiwa ‘mtumbue’, na hapo hapo akatangaza kumsimamisha kazi kwa uchunguzi.

Kitendo hicho kimepingwa na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na utawala bora, ambao walisema  kuwa Rais alitakiwa kwanza kupokea taarifa hiyo na kufanya uchunguzi ambao ungempa Kabwe haki yake ya msingi ya kusikilizwa kabla ya kusimamishwa kwa tamko la hadharani.

Jana, akiongea na viongozi wa ngazi tofauti wa CCM katika hafla ya kuwashukuru kwa kazi waliyoonyesha wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Magufuli alisema kama watu anaowatumbua hadharani pia waliiba hadharani, ni lazima watumbuliwe hadharani.

Magufuli alisema kuwa mateso waliyopata mamilioni ya Watanzania kutokana na kuibiwa, yanafanywa na hao wachache lazima nao waanze kupata mateso hayohayo.

“Kwa hiyo ziko haki za binadamu kwa matajiri tu kwa hawa walioibiwa hakuna haki,” aliuliza Rais Magufuli.

“Kwa hiyo unaweza kuona hawa wanaowatetea nao ni majipu. Tutaanza kuwafuatilia. Hata ukimtoa huyo, nikimsema hadharani wanasema eti nimefanya kosa.

Rais Magufuli alisema kwa bahati nzuri aliwateua yeye na kuwatangaza hadharani, hivyo akahoji sababu za kutotangazwa hadharani siku ya kutenguliwa kwa kuwa ndiyo saizi yake aliyewateua.

“Kama ni mkurugenzi wa manispaa au wa wapi nimemteua mimi. Eti wanasema apewe muda wa kujieleza. Ajieleze yeye aliwapa muda wananchi kujieleza alipokuwa anawaibia? Napenda niwahakikishie tutaendelea kusimama imara,” alisema Dk Magufuli.

==> Zaidi, msikilize kwenye video hii akiongea

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )