Monday, May 16, 2016

12 Wakamatwa Wakituhumiwa Kuhusika na Mauaji ya Watu 7 Jijini Mwanza

Siku chache baada ya watu saba wa familia moja kuuawa kwa mapanga wilayani Sengerema mkoani Mwanza, polisi wamefanikiwa kuwatia mbaroni watu 12 kwa tuhuma za mauaji hayo huku mmojawapo akikamatwa kwa mganga wa kienyeji alikokuwa akijitibu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema hadi jana upelelezi wa tukio hilo lililozua hofu kwa wakazi wa Kijiji cha Sima unaendelea na tayari watuhumiwa 12 wamekamatwa.

“Hakuna jiwe litakalobaki bila kugeuzwa katika upelelezi wa jambo hili, tutawasaka na kuwakamata wote waliohusika kwa njia moja au nyingine na mauaji haya ya kinyama,” alisema Msangi.

Habari zilizopatikana kutoka kwa mtu wa karibu na familia ya marehemu Zakaria Mbata iliyopoteza mama na watoto watatu katika tukio hilo, zinaeleza kuwa wauaji walilenga kupora fedha zilizohifadhiwa kwenye mtandao wa simu.

Pia, chanzo kimoja cha habari kilisema kuwa polisi walimkamata mmoja wa watuhumiwa hao akiwa kwa mganga wa kienyeji alikokuwa akijitibu jeraha alilopata siku ya tukio.

“Katika purukushani za mauaji hayo, huyo mhalifu alijeruhiwa usoni, inaonekana alipigwa na kitu kizito, akakutwa kwa mganga wa kienyeji na amekamatwa kwa mahojiano,” kilisema chanzo hicho
 
Tukio Lenyewe
Usiku wa kuamkia Mei 11, watu wasiojulikana walivamia familia ya Zakaria Mbata na kuua watu saba kwa kuwakata mapanga sehemu mbalimbali za mwili.

Waliouawa katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Augenia Philipo (62), mdogo wake Maria Philipo (56) na watoto wake; Yohana Mabula (20), Regina Aloyce (12) na Mkiwa Philipo (13).

Wageni wawili wa familia hiyo, waliojulikana kwa jina mojamoja ya Donald na Samson nao pia waliuawa katika tukio hilo.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )