Wednesday, May 4, 2016

Kangi Lugola Afurahia Sefue Kutumbuliwa.....Ataka Majipu Sugu Wizara ya Kilimo Yaliyoota Sehemu Nyeti Yatumbuliwe

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola jana alichangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa hisia kali huku akimpongeza Rais John Magufuli kwa kumtumbua Katibu Mkuu Kiongozi.

Ingawa hakumtaja kwa jina, Balozi Ombeni Sefue ndiye Katibu Mkuu Kiongozi aliyeondolewa na Rais Magufuli Machi mwaka huu bila kubainisha sababu ikielezwa kwamba angepangiwa kazi nyingine.

Lugola alisema Rais Magufuli ameonyesha kwa vitendo kuwa anamuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kauli yake kuwa Ikulu ni mahali patakatifu.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo Bungeni mjini Dodoma wakati akichangia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.

Lugola alisema kwa kuwa alikuwa akichangia kwa mara ya kwanza bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano, ni vyema akampongeza Rais kwa namna anavyotumbua majipu kwa ujasiri na bila kupepesa macho.

Lugola akirejea kauli inayosema “kama unataka mali utaipata shambani”, alimtaka Waziri Nchemba kutumbua majipu katika wizara yake. 

“Hatuwezi kupata mali shambani kama hutatumbua majipu kwenye wizara yako ambayo yameota sehemu nyeti .. Rais ametumbua jipu la watumishi hewa. Wizara ya Kilimo ina wakulima hewa na ni jipu ambalo unatakiwa ulitumbue nchi nzima.”

Huku akiungwa mkono na baadhi ya wabunge alisema vocha za pembejeo kwa wakulima ni jipu akisema baadhi ya watumishi wanasajili wakulima hewa na wengine wakiwa ni marehemu na Serikali inaendelea kuwalipa.

Huku akiwataja baadhi yao kwa majina, Lugola alitoa mfano wa kata moja jimboni kwake ambako wakulima hewa wamelipwa vocha zenye thamani ya Sh46.3.

Alisema jipu jingine ni mbegu za pamba aina ya Quton ambazo hazioti akisema zimelalamikiwa na wabunge lakini mwekezaji anakumbatiwa. “Hili ni jipu ikiwezekana ukitoka hapa ukatumbue jipu hili."

Mbunge ahoji kilimo cha mirungi
Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka aliitaka Serikali kuzungumza na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ili kujua ni kwa nini wamehalalisha kilimo cha mirungi.

Alisema Rais huyo ametoa Dola za Marekani milioni mbili, sawa na Sh4 bilioni za Tanzania ili kusaidia ustawi wa kilimo hicho, ambacho kwa Tanzania ni kosa la jinai kulima na kusafirisha.

“Rais Kenyatta ameruhusu kilimo hiki tukizingatia kwamba tuko Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tutahakikishaje kwamba hii mirungi haitaingia kwetu?” alihoji.

Alimtaka Waziri wa Kilimo awasiliane na Kenya ili kujua sababu za kuruhusu kilimo hicho na namna ambavyo wataweza kudhibiti kisilete madhara Tanzania.

Ataka marufuku ya nyavu
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliitaka Serikali kupiga marufuku uzalishaji wa nyavu za kuvulia samaki  ambazo haziruhusiwi badala ya kuwakamata wavuvi. “Kwa nini nguvu kubwa isielekezwe katika kudhibiti uzalishaji wa hizi nyavu. Mpige marufuku uzalishaji wake badala ya kwenda kuzikamata kwa wakulima na kuzichoma,” alisema Serukamba.

Wizara ihame Dar
Mbunge wa Nchemba (CCM), Juma Nkamia alitaka makao makuu ya Wizara ya Kilimo yahame kutoka jijini Dar es Salaam na kwenda katika mikoa yenye mifugo mingi.

Pia aliishauri Serikali kujenga mazingira yatakayovutia kujengwa kwa viwanda vya nyama kwenye mikoa yenye mifugo mingi badala ya kusafirisha mifugo hai umbali mrefu.

Msimamo wa kambi ya upinzani
Akiwasilisha hotuba ya msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, waziri kivuli wa wizara hiyo, Magdalena Sakaya (CUF), alisema itaendelea kulaani ubakaji wa demokrasia Zanzibar.

“Tutaendelea kulaani kubakwa kwa demokrasia kulikotokea huko Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana,” alisema.

Akizungumzia wizara hiyo, Sakaya alisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha asilimia 75 ya machinjio nchini hayana huduma na vifaa vinavyozingatia usafi na ubora wa nyama.

 “Hali hii si nzuri hata kidogo kwa kuwa   magonjwa ya kuambukiza nchini hayataisha kutokana na uchafu uliopo katika machinjio ambayo yanalisha maelfu ya walaji wa nyama,” alisema.

Pia kambi hiyo imeitaka Serikali kupitia upya mikataba yote iliyoingiwa na wawekezaji katika mashamba makubwa kuona kama ina masilahi kwa nchi.

Kambi hiyo ilisema kati ya Sh60.3 bilioni ambazo ziliidhinishwa na Bunge katika mwaka fedha 2015/2016, Sh19.3 zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo hazikupokewa.

Alisema taarifa ya wizara inaonyesha kuwa hadi Machi 31,2016, wizara hiyo ilikuwa haijapokea hata shilingi moja, hivyo akasema hata mipango inayotaka kutekelezwa sasa itakuwa ni ngonjera.

 “Hii mipango ambayo ipo kwenye taarifa ya wizara na ile iliyotolewa katika hotuba ya Waziri Mkuu ni ngonjera tu za kuwafariji wadau lakini ukweli sekta ya mifugo na uvuvi iko mahututi.

"Kambi rasmi ya upinzani inaona kwamba kukua kwa sekta hizi itakuwa ni ndoto kwani hali halisi ni kwamba hakuna fedha za kuendeleza malengo yaliyowekwa katika awamu ya kwanza,” alisema.

Aliikumbusha Serikali kuwa inatakiwa kulipa Sh2 bilioni zilizotokana na amri ya Mahakama kutokana na kesi ya kukamatwa kwa meli ya uvuvi maarufu “samaki wa Magufuli.”

Alisema Serikali inawajibika kulipa fedha hizo kutokana na kufanyika kwa uamuzi ambao haukuzingatia sheria.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )