Sunday, May 8, 2016

Makamu wa Rais: Upinzani Kuna watu makini Wanaoweza Kuikabili Serikali

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonyesha kukerwa na vitendo vya wabunge wa CCM kurusha vijembe na kuutaka Umoja wa Wanawake (UWT) kuwaandalia mafunzo ili waweze kukabiliana na wapinzani ambao alisema wana watu makini na werevu kuweza kukabiliana na Serikali.

Samia, ambaye pia aliweka bayana kuwa chama hicho tawala kilikumbana na upinzani mkali kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua semina ya wabunge, madiwani na viongozi wa CCM wa Mkoa wa Dodoma na baadaye kwenye kikao cha UWT.

Akiwa katika mkutano wa Baraza la UWT, Samia aliwataka viongozi wa jumuiya hiyo kutoa mafunzo maalumu kwa wabunge wapya ili waweze kupambana na wapinzani.

Alihoji ni mambo gani wanayofundishwa wabunge hao wanawake katika kutimiza wajibu wao ndani ya Bunge.

“Tunawafundisha nini ama (tunawafundisha) wakajibu vijembe tu, au wakaseme nini kama wabunge waliotoka UWT?” alihoji.

Samia amesema hayo wakati maneno ya kashfa na vijembe yakizidi kutamalaki ndani ya Bunge na kusababisha kelele, majibizano na wakati mwingine, wabunge wa upinzani kutolewa nje au kususa.

Juzi, wabunge wanawake wa vyama vinavyounda Ukawa walisimama na kupaza sauti kupinga kitendo cha Mbunge wa CCM, Goodluck Mlinga kudai kuwa wanawake wa upinzani hawawezi kupata nafasi za kisiasa bila ya kuitwa “baby”, neno la Kiingereza linalotumika kumaanisha mpenzi.

Naibu Spika Dk Tulia Ackson aliyekuwa anaongoza kikao hicho, alilazimika kuwaamuru wabunge hao waende nje ya ukumbi baada ya kukaidi amri yake ya kuwataka wakae vitini.

Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya mbunge mwingine wa CCM, Augustine Holle kudai kuwa wabunge wawili wa Chadema, Tundu Lissu na John Mnyika wana mafaili kwenye Hospitali ya Mirembe ya mjini Dodoma ambayo inahudumia wagonjwa wa akili na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Kauli yake ilisababisha Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara kunyanyuka kwenye kiti chake na kuanza kumfuata mbunge huyo wa CCM kwa kile kilichoonekana kwenda kupambana naye, lakini hakufanikiwa na kuamriwa aende nje.

Mara kadhaa mbunge mmoja anapokuwa anachangia hoja inayogusa upande mwingine, wabunge huwasha vinasa sauti vyao na kutoa maneno ya kejeli, kashfa na dhihaka yanayosababisha Bunge kujaa kelele za mara kwa mara.

Samia na upinzani 
Akizungumza kwenye kikao na viongozi wa CCM wa mkoa, Samia alisema katika kipindi cha miaka 20 tangu siasa za vyama vingi ziliporejeshwa, vyama vya upinzani vimejijenga na sasa vinaweza kukabiliana na Serikali.

“Bila kusahau kwenye Bunge tuna wenzetu kutoka vyama vya upinzani ambao wamekua vya kutosha, wamepevuka vya kutosha,” alisema Makamu wa Rais.

“Katika miaka 20 ya vyama vingi, upinzani umezalisha watu makini ambao wako tayari kupambana na Serikali. Je, wa kwetu tumewaandaaje katika kupambana nao?”

Kuhusu Uchaguzi Mkuu uliopita, Samia alisema CCM ilipata upinzani mkali kutokana na vyama vya upinzani kuimarika na pia chama hicho tawala kukumbwa na mgawanyiko.

“Kukosa umoja ndani ya chama chetu kulifanya adui akaingia akiwa amejiimarisha na kweli alisumbua sana kwenye uchaguzi na ndiyo maana tunasema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 yaanzie sasa,” alisema Samia.

Alisema kuna baadhi ya viongozi ndani ya chama ambao hawakuwa waaminifu akieleza kuwa ndiyo waliofanya uchaguzi huo uwe mgumu.

CCM ilipoteza makada wawili waliowahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliohamia upinzani na kuwa tegemeo kubwa kwenye kampeni, Lowassa akiwa amepewa nafasi ya kugombea urais na Sumaye akitegemewa kwa hoja zake kwenye mikutano mingi.

Pia, mawaziri, wabunge na madiwani wa CCM walikihama chama hicho na kuimarisha upinzani uliofanya mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kushinda kwa asilimia 58.2, ambao ni mdogo kwa chama hicho kulinganisha na chaguzi zilizopita.

Aliwataka viongozi wa chama kuondoa woga na badala yake waisimamie Serikali kwa kuwa ilani inayotekelezwa ni ya CCM na akawataka wafanye kazi hiyo kwa kushirikiana na watu wa chini yao.

Akiwa kwenye mkutano wa jana, Samia alisema UWT haina budi kukaa na wabunge hao na kufanya nao mafunzo maalumu kwa sababu kazi kubwa ya makundi ya wanawake ndani ya mabaraza ya kutunga sheria ni kutetea masilahi yao.

Sophia Simba ataka wakuu wa Wilaya
Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba alimuomba Makamu wa Rais kuwaombea kwa Rais Magufuli kuwapa kipaumbele wanawake wengi katika nafasi za ukuu wa wilaya wakati atakapofanya uteuzi akisema wana uwezo mkubwa wa kutumikia nafasi hiyo.

Alisema UWT itakuwa na shughuli mbalimbali ambazo itafanya kwa muda wa siku tatu mkoani Dodoma, ikiwa ni pamoja na kumpongeza Samia ambaye pia ni mmoja wa wadhamini wa umoja huo, kwa kuchaguliwa kwake kushika nafasi hiyo.

Majipu yatatumbuliwa 
Akizungumzia suala la kutumbua majibu, Makamu wa Rais alisema kazi hiyo itaendelea hadi wahakikishe Taifa linarudi kwenye mstari na akaomba viongozi wote kuwa makini katika sehemu zao za kazi. 

“Hapa napo niseme ukweli kuwa majipu siyo tu yapo huko juu, hata katika ngazi za chini yapo tena kuanzia kwenye chama na Serikali. Anzeni kuyatumbua kwa kuwa mkichelewa mtatumbuliwa ninyi,” alisema.

Aliwataka kujiandaa kwa kuwa “mzee wa kutumbua majipu” yupo karibu kukabidhiwa chama ambacho alisema kina majipu.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )