Monday, May 9, 2016

Mbunge Alaani Matusi na Udhalilishaji Bungeni


MBUNGE wa Siha (Chadema), Godwin Mollel, amelaani lugha chafu zinazotumika bungeni ambazo zinawazalilisha wanawake na kwamba kitendo hicho kinashusha hadhi ya Bunge.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizindua kitabu cha siri za utumishi madhabahuni kilichotungwa na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mikaeli Memiri.
 
Aliwataka wanafunzi kuwa na nidhamu ili watakapobahatika kuwa wabunge wazingatie maadili na kuwatumikia wananchi.
 
Alisema kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya wabunge kumesababisha kuwapo lugha za uzalilishaji dhidi ya wanawake, jambo ambalo linatakiwa kukemewa.
 
Alisema kuna mila ambazo zinamkandamiza mwanamke katika kupata uongozi kwa kudhani kuwa nafasi hiyo inatolewa kwa njia ya ngono, jambo ambalo sio la kweli.
 
Kuhusu kitabu alichozindua, Mollel alisema mwandishi ameonyesha udhubutu, hivyo kuna haja ya serikali kuwasaidia vijana kama hao ili waweze kukua kiuchumi pamoja na kufahamika.
 
Alisema mara nyingi watungaji wa vitabu hawathaminiki huku baadhi ya watu wakitumia mawazo yao kujinufaisha huku wahusika wakiendelea kubakia maskini.
 
Aliahidi kumsaidia mwanafunzi huyo ambaye ametumia muda mwingi kutunga kitabu hicho ambacho kitasaidia kuielimisha jamii.
 
Naye Memiri alisema lengo la kutunga kitabu hicho ni kutaka kubadilisha fikra za jamii pamoja na kufikia malengo yake ya kuwasaidia wanaoishi katika mazingira magumu.
 
Alisema amepitia shida nyingi katika maisha yake lakini licha ya changamoto alizokuwa nazo ikiwamo kusomesha watoto wawili, alitumia mkopo wake aliopatiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutunga kitabu hicho.
 
Alisema anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa ofisini, vitendea kazi kama mashine za kuchapishia vitabu na hivyo kufanya shughuli zake katika mazingira magumu.
 
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Mtakatifu Peter Clavery, Oswald Nyinge, alisema mara nyingi serikali inawathamini watungaji wa vitabu ambao ni maprofesa wakati ni sehemu yao ya kazi na kuwapuuza waandishi wachanga hali inayowakatisha tama, hivyo kuna haja ya serikali kuwatambua pamoja na kuwaongezea uwezo.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )