Tuesday, May 17, 2016

Serikali: Hatuna Msamaha na Wauza Madawa ya Kulevya

Serikali  imesema haitakuwa na msamaha wala suluhu kwa wahusika wote wa biashara haramu ya dawa za kulevya. 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alitoa rai kwa watu wote kutojihusisha na uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa hizo.

Kitwanga aliyasema hayo jana bungeni mjini hapa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Alisema, tatizo la biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya limeendelea kuwepo nchini na katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016, kilogramu 141.7 za dawa za kulevya za viwandani ambazo ni heroin, cocaine, cannabis resin, morphine na mandrax zilikamatwa na watuhumiwa 719 (wanaume 644 na wanawake 75) walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Aidha, kilo 18,513 na gramu 415 za bangi na kilo 15,402 za mirungi zilikamatwa ambapo watuhumiwa wanaume 9,935 na wanawake 1,020 walikamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema.

Alisema, katika mwaka 2016/17 Jeshi la Polisi litaendeleza mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kubaini mtandao wa wahalifu wa ndani na nje ya nchi unaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.

Akizungumzia vita dhidi ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, alisema wizara ilianzisha Sekretarieti ya Kupambana na Kudhibiti Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu kwa lengo la kudhibiti biashara hiyo.

Kitwanga alisema hilo lilifanyika baada ya ripoti mbalimbali za kitaifa na kimataifa kuitaja Tanzania kama chanzo, njia ya kupitishia na kituo cha mwisho kwa biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Alisema katika mwaka 2015/16 sekretarieti hiyo ilizuia hati na nyaraka za kusafiria za wasichana 31 wa Tanzania kwa lengo la kufanya uchunguzi kubaini mtandao wa wasafirishaji haramu wa binadamu. 

Alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 Sekretarieti imejipanga kufanya ufuatiliaji na uchunguzi wa wazi juu ya biashara hiyo.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )