Saturday, June 11, 2016

BoT imetoa Sh. Milioni 273 kuchangia ununuzi wa madawati nchini.

Hussein Makame-MAELEZO
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na wafanyakazi wake wa matawi yote nchini kwa kushirikana na baadhi ya Taasisi za kifedha na kampuni za simu nchini, imetoa Shilingi Milioni 273 kuchangia ununuzi wa madawati ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Benki hiyo.

Fedha hizo zilikabidhiwa leo kupitia hundi ya mfano kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya matembezi ya hisani yaliyolenga kuchangia madawati, yaliyoanzia Ofisi za BOT hadi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kukabidhi fedha hizo, Gavana wa BOT Prof. Benno Ndulu alisema lengo la mchango huo ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza ubora wa elimu kupitia upatikanaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.

“Tunatambua kwamba changamoto hiyo (uhaba wa madawati) ni kubwa, lakini tunaamini mchango wetu utasaidia kupunguza makali ya tatizo hilo na kuongeza idadi ya watoto wetu ambao wanasoma wakiwa wamekaa kwenye madawati” alisema Gavana Prof. Ndulu

Akifafanua mchango huo, Gavana Prof. Ndulu alisema kati ya fedha hizo, BOT imetoa Shilingi Milioni 167, Wafanyakazi Milioni 29.8, Taasisi za Kifedha Milioni 22 na kampuni za simu Milioni 54.3 na kwamba madawati hayo yatasambazwa kwenye shule zenye upungufu au ukosefu wa madawati za Dar es Salaam na zilizoko mikoa ambayo Benki hiyo ina matawi yake.

Alitaja mikoa hiyo na fedha zilizochangwa na wafanyakazi wa BOT wa matawi ya mikoa hiyo kuwa ni Makao Makuu Dar es Salaam waliochangia Shilingi Milioni 22, Mwanza (Milioni 1.24), Chuo cha Benki Mwanza (680,000) Arusha (Milioni 1.23) Mbeya (Milioni 1.186), Mtwara (850,000) na Dodoma (Milioni 1.18).

Alisema taasisi zilizochangia fedha hizo ni Benki ya India Shilingi Milioni 5, Benki ya Habib (Milioni 5), Benki ya Exim (Milioni 5), Benki ya UBA (United Bank for Africa, Milioni 2), Tanzania Mortgage Refinance (Milioni 2), China Community Bank (Milioni 2) na NIC Bank aliyotoa Milioni 1.

Kwa upande wa kampuni za simu zilizotoa fedha ni kampuni ya Vodacom iliyotoa Dola za Kimarekani 10,000, kampuni ya Tigo Dola za Kimarekani 10,000 na kampuni ya Selcom iliyotoa Dola za Kimarekani 5,000.

Akizungumza baada ya kupokea hundi ya mfano, Waziri Mkuu Majaliwa alisisitiza fedha hizo zitumike kama zilivyokusudiwa na yeyote atakayetumia fedha hizo kinyume na malengo achukuliwe hatua mara moja.

Katika kuthamini sekta ya elimu nchini, Gavana Prof. Ndulu alisema benki hiyo ilianzisha Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambapo hadi sasa umetoa ufadhili kwa wanafunzi 22 kusoma shahada za kwanza na za uzamivu katika vyuo vikuu hapa nchini katika masomo ya sayansi, hisabati, uchumi, fedha, uhasibu na TEHAMA.

“Lengo kubwa la mfuko huu ni kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na hisabati yakiwemo masomo kuhusu gesi na mafuta.Katika idadi hiyo, 16 ni wanafunzi wa kike na waliobaki 8 ni wanaume” alisema Gavana Prof. Ndulu.

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ilianza kutoa huduma kwa wananchi mnamo tarehe 14 Juni mwaka 1966 na Juni 14 mwaka huu inatimiza Miaka 50 na katika kuadhimisha miaka hiyo wafanyakaz wa matawi yote nchini wanafanya matembezi hayo ili kutoa mchango kwa jamii.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )