Tuesday, June 14, 2016

Mahakama Ya Kisutu Yatengua Udiwani Wa Chadema Kata Ya Saranga


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetengua matokeo ya kiti cha  diwani wa Kata ya Saranga, Efraim Kinyafu (CHADEMA),  baada ya kubaini kwamba uchaguzi ulikiuka taratibu katika  kuhesabu kura.

Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Mdoe dhidi ya diwani huyo Kinyafu na msimamizi wa uchaguzi wa kata hiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hukumu hiyo imetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema ambaye kwa sasa amehamishiwa kituo kingine cha kazi na ilisomwa kwa niaba yake na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

“Mahakama baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, imebaini kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika kuhesabu kura inatengua matokeo ya uchaguzi wa kata ya Saranga” alisema Hakimu Mashauri.

Mdoe alifungua kesi hiyo akidai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kuhesabu kura akilalamikia kituo kimoja na kuiomba mahakama kuamua vyovyote itakavyoona inafaa na itamke uchaguzi haukuwa wa huru na wa haki.

Akizungumza baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Fredrick Kihwelu, alidai mteja wake hajaridhika na hukumu hiyo hivyo watakata rufani kuipinga.

Alidai wataomba mahakamani wapatiwe mwenendo wa kesi ili waweze kuwasilisha sababu za kukata rufani.

Wakili huyo alidai mdai huyo alikuwa halalamikii kushindwa kwa kuwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, alikiri kushindwa kwa tofauti ya kura zaidi ya 500.

Alidai katika kituo ambacho alikuwa akilalamikia mdai huyo kulikuwa na wapigakura 68, hivyo hata kama kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kuhesabu kura kusingeweza kubadili matokeo yote.

Wakili huyo alishauri kwamba aliyepaswa kusahihishwa kwa kukiuka taratibu ni  Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kesho na keshokutwa iwe makini kwa kutorudia  makosa na sio mdaiwa wa kwanza (Kinyafu).

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )