Friday, June 3, 2016

Mama Janeth Magufuli amshukuru TB Joshua kwa kuuunga mkono jitahada zake za kusaidia wazee.

Mke wa Rais, Janeth Magufuli amewaomba viongozi kusimamia na kuhakikisha misaada yote inayotolewa kwa ajili ya wazee na watu wenye mahitaji maalumu inawafikia walengwa.

Pia, alimsifu mhubiri wa Nigeria, TB Joshua kwa kujitoa katika kuwasaidia wazee na watu wasiojiweza nchini huku akiitaka jamii iige mfano huo.

Mama Magufuli alisema hayo alipokuwa akitoa misaada katika Kituo cha Kaseka cha Wazee na Walemavu wa Ukoma kilichopo wilayani hapa Mkoa wa Mtwara.

“Niombe viongozi waliopo hapa kuhakikisha walengwa wanafaidika na misaada wanayopata, tayari nimepata malalamiko mengi kutoka kwa Wasukuma wenzangu kule Mwanza, yanavunja moyo.

‘‘Naomba watu wasiuze wala kuiba ni dhambi kubwa ukichukua chakula cha mtu mwenye mahitaji na asiyejiweza hiyo laana itakufuatilia kwa sababu ni sadaka ishaombewa,” alisema.

Mama Magufuli kwa kushirikiana na Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa walikabidhi misaada mbalimbali ikiwamo vyakula, nguo, saruji, vitanda na magodoro ambavyo vimetolewa na TB Joshua, kampuni ya Super Doll, Dangote na viongozi wanawake wa Mkoa wa Mtwara.

“Niombe wizara, taasisi, Serikali na mashirika ya ndani na nje kuiga mfano wa TB Joshua kwani hakuangalia utaifa wala dini, uwapo wetu hapa unaonyesha ni namna gani nchi na mila zetu za Kitanzania zinavyothamini na kuheshimu wazee na watu wenye mahitaji maaalumu,” alisema Mama Magufuli.

Mwenyekiti wa wazee hao, Cosmas Mbego aliwashukuru waliotoa misaada hiyo akisema wanashangazwa kwani hawakuwahi kutembelewa na wake wa viongozi waliopita.

“Lakini niseme ukweli maji huwa hatupati. Mlipokuja ninyi yanatoka lakini mtakapoondoka watayafunga,” alisema Mbego 

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego aliwahakikishia wazee hao kuwa tatizo la maji limeondoka na watakapoondoka yataendelea kutoka.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )