Tuesday, June 14, 2016

Mbunge Tundu Lissu na Mwandishi Simon Mkina wafikishwa Mahakamani kwa kuandika makala ya kichochezi


PETER Kibatala wakili wa upande wa washitakiwa katika kesi inayowakabili waandishi wa gazeti la MAWIO na watu wengine wawili akiwemo mbunge Tundu Lissu, wameifanya serikali  iombe siku 14 ili kujipanga kujibu hoja zake.

Katika kesi hiyo ya uchochezi ambayo, mshitakiwa wa kwanza ni Jabir Idrissa mwandishi mwandamizi wa gazeti la MAWIO huku Simon Mkina ambaye ni mhariri wa gazeti hilo akiwa ni mshitakiwa wa pili.

Aidha Ismail Mahboob, mchapishaji wa gazeti hilo ni mshitakiwa wa tatu na Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) anayedaiwa kutoa taarifa za uchochezi zilizochapwa na MAWIO akishitakiwa kama mshitakiwa wa nne.

Akisoma mashtaka hayo Paul Kadushi, Wakili wa Serikali Mbele ya Thomas Simba, hakimu Mkazi mahakama ya Kisutu amesema watu hao wanashitakiwa kwa makosa matano.

Shitaka namba moja ni la kupanga njama za kutoa chapisho la uchochezi, kosa linalodaiwa kutendwa kati ya tarehe 12 na 14 Januari mwaka huu ambapo;

Idrisa, Mkina na Lissu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam walipanga njama za kuchapisha taarifa za uchochezi kinyume na sheria ya magazeti kifungu cha 32(1)(a).

Shitaka namba mbili linawakabili pia mwandishi Idrissa, mhariri Mkina na mbunge Lissu,  kwa kuandika habari za uchochezi zilizochapwa katika gazeti la MAWIO toleo namba 182 yenye kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar.”

Shitaka la tatu linamkabili mshitakiwa namba tatu Ismail Mehboob ambapo, anatuhumiwa kuwa, 13 Januari katika jengo la Jamana, Ilala alichapisha gazeti la MAWIO lenye habari ya uchochezi kinyume na sheria ya magazeti kifungu cha 32 (1) (c).

Shitaka la nne linamkabili pia mtuhumiwa namba tatu (Mehboob) kwa kuchapisha gazeti hilo bila kuwasilisha hati ya kiapo kwa msajili wa magazeti kinyume na sheria ya magazeti kifungu namba 6 na 12 (a).

Katika kosa la tano, mshitakiwa namba moja (Idrissa), namba mbili (Mkina) na namba nne (Lissu), wanatuhumiwa kuchochea hofu miongoni mwa wananchi kwa kuchapisha habari “Machafuko yaja Zanzibar” na kwamba habari hiyo ingeweza kuzua vita au umwagaji damu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshitakiwa namba mbili (Mkina) na namba tatu (Mehbooob) walikana mashitaka yao huku mshitakiwa Idrissa na Lissu wakishindwa kufika mahakamani kutokana na sababu mbalimbali.

Hata hivyo Peter Kibatala wakili wa washitakiwa ameiomba mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo kwa madai kuwa haina mashiko yoyote kisheria.

Kibatala amefafanua kuwa, kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kifungu cha 89 (A) mtu hawezi kushitakiwa kwa kosa la uchochezi bila idhini ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka ya serikali (DPP).

Huku akiongeza kuwa kati ya mashitaka yote matano ambayo serikali imeyawasilisha mahakamani ni shitaka moja tu (la tatu) ndilo lenye idhini ya DPP na hivyo akaiomba mahakama kufuta shitaka namba moja, mbili, nne na tano.

Wakili huyo aliomba mahakama pia kulifuta shitaka la tatu kwani licha ya kuwa na idhini ya DPP lakini linakosa mashiko kwasababu lipo nje ya wigo wa kisheria uliowekwa na sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.

Kibatala amesema sheria ya magazeti namba 4 ya mwaka 1976 kifungu cha 31(2) a,b,c,d inafafanua kuwa, “Kitendo, maneno au chapisho halitakuwa la uchochezi ikiwa litakuwa linaonesha mapungufu au makosa ya serikali na kuitahadharisha ijisahihishe.”

Huku akihitimisha hoja zake kwa kusema, mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu haina uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo kwa kuwa washitakiwa wanashitakiwa kwa kosa la kuchochea uvunjifu wa amani visiwani Zanzibar.

“Sheria ya magazeti ya 1976 siyo sheria ya Muungano, Zanzibar wanayo sheria yao ya magazeti kwahiyo mahakama hii haiwezi kusikiliza mashitaka haya kwasababu yanahusu uchochezi wa uvunjifu wa amani Zanzibar.” Alihitimisha Kibatala.

Mawakili wa upande wa serikali wakiongozwa na Paul Kadushi walipopewa nafasi ya kujibu hoja zilizotolewa na wakili wa washitakiwa, waliiomba mahakama kuwapa siku 14 ili kuweza kujipanga kujibu hoja hizo.

Ombi lililokubaliwa na Hakimu Thomas Simba pamoja na wakili Kibatala na hivyo kesi hiyo kuahirishwa mpaka 28 Juni 2016, saa tano kamili asubuhi ambapo itatajwa tena.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )