Thursday, June 30, 2016

Mvutano Mkali Waibuka Wakati wa Kupitisha Muswada wa Marekebisha ya sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2016


Serikali imejikuta katika wakati mgumu wakati wa upitishaji wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016 baada ya wabunge kupinga baadhi ya hatua zilizochukuliwa katika muswada huo. 

Jana, Bunge lilitumia zaidi ya saa mbili kupitisha muswada huo huku mvutano ukiibuka katika nyongeza ya mapendekezo ya ununuzi wa dawa na vifaatiba kufanywa kwa dharura na kupinga kwa kamati za fedha na mipango kuondolewa katika kusimamia mchakato wa zabuni kwenye halmashauri. 

Mashambulizi hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia na wabunge Joseph Kakunda (Sikonge CCM), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini CCM) na Andrew Chenge wa Bariadi Magharibi (CCM), kiasi cha kumfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kukubali baadhi ya mapendekezo ya Bunge kwa shingo upande. 

Hii ni mara ya kwanza kwa wabunge wa CCM kuipinga vikali Serikali kwa kura wakati wa kupitisha vifungu na kufanya Bunge lirudishe uhai wa mjadala tangu Ukawa waanze kususia vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson. 

Awali, katika mjadala wabunge wengi walipongeza hatua ya Serikali kupunguza muda na gharama za mchakato wa zabuni, ushirikishaji wa makundi maalumu katika jamii kwenye zabuni za umma lakini walipinga uamuzi wa kuwaondoa madiwani katika mchakato wa ununuzi. 

Katika kifungu cha 11 cha muswada huo, Serikali ilikusudia kuondoa jukumu la kamati ya fedha na mipango katika usimamizi wa masuala ya ununuzi ya halmashauri. 

Kabla ya Bunge zima kukaa kama kamati kupitisha muswada huo, Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango alieleza kuwa Serikali ilikuwa imeridhia kurudisha jukumu la kamati hizo ambazo huundwa na madiwani kuwasimamia watendaji watakaoshindwa kutekeleza kazi zao. 

Licha ya Serikali kukubali hoja hiyo, wabunge bado waliitaka kuingiza maana katika kifungu cha pili na kuweka maboresho kifungu cha 24 ili vifaatiba na dawa vinunuliwe kwa dharura huku Masaju akipinga kwa maelezo kuwa suala hilo lingeingizwa kwenye kanuni atakazotunga waziri. 

Ghasia alieleza kuwa vifaatiba na dawa ni muhimu katika kuokoa maisha ya binadamu hivyo ni vyema kianzishwe kifungu maalumu katika sheria badala ya kubaki katika kanuni na kusubiri majaliwa ya waziri. 

Kitendo cha Masaju kupinga pendekezo hilo, kiliwafanya wabunge, Chenge, Sophia Simba (Viti Maalumu) na Kangi Lugola wa Mwibara kusimama wakisema Serikali inataka kupitisha mambo kibabe. 

“Kila siku sheria zinakuwa mbaya kwa sababu maoni ya wabunge yanapuuzwa. Serikali ikitaka mambo yake yapite inalazimisha, haiwezekani. Dawa ni maisha, AG kubali hili na likileta shida mtaleta turekebishe mbona mengine huwa mnaleta tunarekebisha?” alisema Lugola. 

Chenge alisema Serikali ingekuwa imeipatia muda kamati ya bajeti imalize kazi zake, kusingetokea mvutano kwa kuwa mengine wangejadiliana na kuyamaliza. 

Mvutano huo ulimfanya Ghasia kuhamia kwenye meza ya Chenge ili kupata ushauri wa kisheria na hata wakati mwingine kusahau na kumweleza Naibu Spika kuwa baadhi ya masuala angeeleza mwanasheria wake (Chenge). 

Pamoja na Serikali kukataa mapendekezo hayo, wabunge walipigia kura ya ‘Ndiyo’ maboresho ya kamati na kuwaacha Masaju na Dk Mpango wakitikisa vichwa kwa masikitiko. 

Hoja nyingine iliyomfanya Masaju kususia kuendelea kutetea ni ile ya Profesa Tibaijuka iliyopitishwa na wabunge ya kuongeza maneno yatakayowataka wazabuni wa kimataifa kuhusisha wazawa katika kifungu cha 18 cha muswada. 

“Msitunge Sheria kwa hasira. Hiki kifungu kitakuwa kigumu kutekelezeka. Tungeni hivyo lakini mjue itakuja kuleta shida,” alisema Masaju akionyeshwa kukerwa na kilichofanywa na wabunge na kueleza maneno hayo tayari yalikuwapo kwenye Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2011 inayoboreshwa. 

Sehemu nyingine iliyoleta mjadala ni pendekezo la Kamati ya Bajeti kuongeza kifungu cha kuanzisha akaunti maalumu ya ununuzi mdogo mdogo utakaozisaidia taasisi za umma kutumia wataalamu wa ndani na kununua vifaa vya marekebisho madogo kama kurekebisha vyoo na vitasa. 

Masaju alipinga pendekezo hilo akisema litafungua ufisadi katika halmashauri jambo ambalo wabunge wamekuwa wakilalamikia kila siku. 


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )