Thursday, June 9, 2016

Mwanza, Kagera, Kigoma Zaongoza kwa Umasikini wa Kipato


PAMOJA na maendeleo yaliyotokana na kukua kwa pato la wastani la Mtanzania na kupungua kwa umasikini wa mahitaji ya msingi, serikali imeainisha mikoa mitano iliyokithiri kwa umasikini wa kipato.

Akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi ya 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema mkoa unaoongoza ni Kigoma ambao wakazi wake asilimia 48.9, wanakabiliwa na umasikini uliokithiri wa kipato.

Mikoa mingine yenye umasikini wa kipato kiwango chake katika mabano ni Geita (asilimia 43), Kagera (asilimia 39), Singida (asilimia 38.2) na Mwanza (asilimia 35.3). 

Katika wilaya zilizokithiri kwa umasikini wa kipato, ni Kakonko mkoani Kigoma na Biharamulo mkoani Kagera, ambapo Dk Mpango alisema katika wilaya hizo, takribani asilimia 60 ya watu wake, wako chini ya mstari wa umasikini wa mahitaji ya msingi.

Tathmini ya hali ya umasikini kimaendeleo iliyoainisha umasikini huo, imetumia takwimu za Sensa ya Watu ya mwaka 2012 na Utafiti wa Hali ya Kipato na Matumizi katika Kaya wa 2012, ulionesha pia ahueni ya umasikini katika mikoa mitano.

Dk Mpango alitaja mikoa hiyo yenye ahueni na idadi ya watu wanaokabiliwa na umasikini wa kipato katika mabano kuwa ni Dar es Salaam (asilimia 5.2), Kilimanjaro (asilimia 14.3), Arusha (asilimia 14.7), Pwani (asilimia 14.7) na Manyara (asilimia 18.3). 

Pamoja na tathmini ya kimkoa na kiwilaya lakini katika nchi nzima, alisema kati ya mwaka 2010 na 2015, Pato la Mtanzania liliongezeka kutoka Sh 770,464.3 kwa mwaka mpaka Sh milioni 1.9 mwaka 2015 sawa na mara 2.5.

Aidha kupungua kwa umasikini nako kulikuwa kasi katika kiwango cha asilimia 6.2 ndani ya miaka mitano tu kati ya mwaka 2007 na 2012, ikilinganishwa na kupungua kwa umasikini kwa asilimia 4.6 tu katika miaka 15 kulikotokea mwaka 1992 mpaka 2007.

Kuhusu ajira, Dk Mpango alisema Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 ulionesha kuwa nguvukazi ya Taifa ilikuwa watu 25,750,116 sawa na asilimia 57 ya watu wote wa Tanzania Bara.

Kati ya nguvu kazi hiyo, wanawake wametajwa kuwa 13,390,678 sawa na asilimia 52 na wanaume ni 12, 359, 438 sawa na asilimia 48. 

Pamoja na nguvukazi kuwa watu milioni 25.8, utafiti huo kwa mujibu wa Dk Mpango, ulionesha kuwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi walikuwa watu milioni 22.3 tu na sababu za watu kushindwa kufanya kazi zilikuwa ni ulemavu na ugonjwa wa muda mrefu.

Aidha, kati ya nguvu kazi ya taifa; watu milioni 25.8, utafiti huo umeonesha kuwa asilimia 77.8 ndio walikuwa katika ajira, wengi wakiwa wa vijijini sawa na asilimia 82.2 ikilinganishwa na mijini ambapo Dar es Salaam waliokuwa wakifanya kazi ni asilimia 59.8 tu.

Mafanikio ya kupungua kwa umasikini, yameonekana pia katika kuongezeka kwa umri wa kuishi wa Mtanzania kutoka miaka 51 ilivyokuwa mwaka 2001 mpaka miaka 61 kwa takwimu za mwaka 2012.

Vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja, pia vimepungua kufikia 43 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2015 kutoka vifo vya watoto 51 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2010.

Kuhusu watoto wa chini ya miaka mitano, pia vifo vyao vimepungua kutoka vifo vya watoto 81 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2010 mpaka vifo vya watoto 67 kwa kila watoto hai 1,000 mwaka 2015.

Mafanikio hayo ya kupungua kwa vifo na kuongezeka kwa umri wa kuishi wa Mtanzania, katika upande mwingine yameleta changamoto kutokana na kuongezeka kwa wasichana waliopata ujauzito utotoni.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, idadi ya wasichana wanaopata mimba katika umri wa miaka 15 hadi 19 imeongezeka na kufikia asilimia 27 mwaka 2015, kutoka asilimia 23 mwaka 2010.

Dk Mpango alisema hali hiyo si dalili nzuri kwani kunaashiria kuongezeka kwa utegemezi na kudumaza jitihada za kuondoa umasikini katika jamii na kuwataka wabunge kushirikiana na Serikali kuhimiza watoto wa kike, kuongeza bidii katika masomo ili kwa pamoja kupatikane manufaa kutokana na mapambano ya umasikini.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )