Saturday, June 4, 2016

Serikali Kutoajiri Madaktari Watakaotaka Kufanya Kazi Mjini Pekee


SERIKALI imetangaza msimamo wake wa kutoajiri madaktari watakaotaka kufanya kazi katika maeneo ya mijini pekee hususan Dar es Salaam, badala yake imesema itawachukua watakaokuwa tayari kuhudumia wagonjwa katika maeneo yote ya nchi.

Aidha, imeonya tabia ya baadhi ya madaktari bingwa kung’ang’ania kufanya kazi mijini na kusema wanawanyima haki wahitaji wa huduma zao katika maeneo ya mengine tofauti na mijini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitoa msimamo huo jana bungeni mjini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM) aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupeleka madaktari bingwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora aliyotajwa ina uhaba mkubwa wa madaktari hao.

Ummy alisema, “Madaktari wanaoomba kazi wajiandae kutawanywa na wajue kuwa sasa hatutachukua watakaotaka kukaa mijini hasa Dar es Salaam, kwa kuwa wananchi katika maeneo mengine yasiyo ya mijini wanahitaji huduma zao pia, hasa madaktari bingwa wa wanawake.”

Alisema anatambua changamoto ya uhaba wa madaktari katika hospitali ya mkoa wa Tabora na kwamba utapewa kipaumbele mwaka huu Serikali itakapoanza kutekeleza mpango wa kupeleka madaktari bingwa kwenye mikoa tisa nchini.

“Tabora imefanyiwa tathmini ikabainika ina uhaba wa madaktari, mwaka huu itapatiwa madaktari kwa sababu tuna mpango wa kuwapeleka katika mikoa nane na huo sasa utakuwa ni wa tisa na utapewa kipaumbele,” alisema Ummy.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Suleiman Jaffo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Raphael Michael alisema, ili kuhakikisha ukarabati wa miundombinu ya hospitali ya Mawenzi unafanyika, Serikali imetenga Sh bilioni 1.35 katika bajeti yake ya mwaka 2016/17.

Katika swali lake la msingi lenye vipengele a, b na c, Michael aliuliza ni lini hospitali hiyo itafanyiwa ukarabati iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuiongezea madaktari na wauguzi.

Aliuza pia ni lini Serikali itakubali ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi la kujenga hospitali ya wilaya na je, Serikali itasaidiaje hospitali ya Mawenzi iweze kupata mkopo kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), ili iweze kuboresha miundombinu yake.

Akijibu alisema, mkoa umejiwekea utaratibu wa kufanya ukarabati wa hospitali ya mkoa kupitia fedha za uchangiaji gharama za matibabu.

Hadi sasa zimetumika Sh 14,700,000 kwa ajili ya ukarabati wa mfumo wa maji, jengo la wagonjwa wa nje pamoja na jengo la madaktari waliopo mafunzoni na kuongeza kuwa mkakati uliowekwa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili kujenga uwezo wa kuihudumia hospitali hiyo.

Kuhusu suala la watumishi, alisema hospitali hiyo imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya 79 katika mwaka 2015/17 na watumishi 65 wamepangwa kuajiriwa katika mwaka ujao wa fedha ili kukabiliana na upungufu uliopo.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )