Tuesday, June 7, 2016

Wabunge wa Upinzani Wanaosusia Vikao vya Bunge Wataendelea Kulipwa Posho Zao


Udhaifu wa Kanuni za Bunge katika kufafanua mambo mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge, umeelezwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwa unatakiwa kurekebishwa ili kutoa nafasi ya Kiti cha Spika kutoa uamuzi dhidi ya vitendo visivyokubalika vinavyoendelea ndani ya Bunge.

Amesema hayo jana alipokuwa akitoa majibu wa muongozo alioombwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) kuhusu uhalali wa posho wanazolipwa wabunge wa Kambi ya Upinzani, ambao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kwenda kupumzika.

Dk Tulia alisema tangu Mei 30, mwaka huu, wabunge hao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kuondoka kwenda kupumzika, jambo lililosababisha Dk Mwakyembe kuomba muongozo kama malipo hayo ni haki kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya Katiba ya 23.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo ya kwanza na ya pili; “Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya.Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.” 

Akitoa muongozo wake kama malipo hayo ya posho ni halali kwa mujibu wa Katiba au la, Naibu Spika alisema ametumia uamuzi wa Kiti cha Spika uliotolewa Aprili 27, 2016 kuhusu muongozo kama huo.

Alisema Kiti cha Spika katika muongozo huo wa Bashe, kilinukuu Katiba Ibara ya 73 inayosema, “Wabunge wote wa aina zote watashika madaraka yao kwa mujibu wa Katiba hii, na watalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”

Mbali na malipo hayo kulindwa na Katiba, Dk Tulia alisema pia Sheria ya Uendeshaji wa Bunge Sura ya 15 na 19 Kanuni za Bunge zinaelezea kuwa mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge, atalipwa posho.

Dk Tulia alisema vitendo vya kutohudhuria mjadala wa Bunge havikubaliki kwa kuwa havikidhi matakwa ya Katiba Ibara ya 23, lakini akasema pamoja na Kiti cha Spika kusisitiza kuwa kutohudhuria mjadala hakukubaliki, lakini kuna haja ya kubadili sheria ili mbunge alipwe baada ya kumaliza kazi.

Pia alisisitiza kuwa Kanuni za Bunge zinazotumika katika kuwalipa posho, hazijaeleza kwa uwazi maana ya neno mahudhurio, hivyo nazo zinahitaji marekebisho kudhibiti hali hiyo.

Baaada ya kutoa muongozo huo, Keissy alisimama na kuomba muongozo mwingine na alipopewa nafasi, aliomba utaratibu wa kutumia mashine za kielektroniki kusaini mahudhurio, ubadilishwe na badala yake urejeshwe ule wa zamani wa mbunge kusaini katika karatasi.

Dk Tulia akijibu muongozo huo, alisema hata ukirejeshwa utaratibu huo, mbunge anaweza kusaini katika karatasi saa tano na kuondoka kwenda Dar es Salaam na kusisitiza kunahitajika marekebisho ya Kanuni za Bunge ili neno mahudhurio, lipewe ufafanuzi wa wazi.

Hata hivyo, aliahidi kuwasiliana na Katibu wa Bunge ili kuona utaratibu mzuri wa wabunge kusaini posho katika wakati wa sasa. 

Baada ya muongozo huo wa Naibu Spika, Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu alidai wao wataendelea kususia vikao vyote vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika kwa madai kuwa anatumia Kanuni za Bunge, kuwakandamiza.

Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni, Mbilinyi alisema wabunge wa Kambi ya Upinzani wanaposusa hawarudi nyumbani kupumzika, bali wanashinda katika maktaba ya Bunge kufanya kazi.

Mbilinyi alisema ni heri wabunge wa Kambi ya Upinzani wanaoshinda katika maktaba ya Bunge, kuliko wa CCM wanaohudhuria vikao hivyo.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )