Monday, June 6, 2016

Waziri Mkuu : Mataifa Yaliyoendelea Yashirikiane Na Serikali Ya Tanzania Kuwahudumia Wakimbizi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameyaomba mashirika ya Kimataifa na Nchi zilizoendelea zishirikiane na Serikali ya Tanzania katika kuwahudumia wakimbizi.

“Kwa sasa tunashirikiana na UN (Umoja wa Mataifa) kuwahudumia wakimbizi, hivyo tunaomba mataifa mengine nayo yatusupport katika jambo hili,” amesema.Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 6, 2016) alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Mhe. Dibr Reynders ofisini kwake Bungeni, Dodoma.

Amesema Tanzania inahifadhi jumla ya wakimbizi 165,000 kati ya 230,000 walioko katika nchi za Maziwa Makuu, ambapo bajeti ya Serikali haitoshelezi kuwapa huduma wanazostahili.Waziri Mkuu Majaliwa amesema wakimbizi hao wanaishi kwenye kambi mbalimbali nchini zikiwemo za Nyarugusu na Nduta zilizoko wilayani Kasulu na Kibondo ambazo alizitembelea Desemba mwaka jana.

Amesema wakimbizi hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za uhaba wa maji safi, ufinyu wa huduma za afya na elimu na uharibifu wa mazingira .Amesema wengi wa wakimbizi hao ni raia wa Burundi, Kongo na Rwanda, pia amemuomba Mhe. Reynders atakapofika Burundi akahamasishe amani.

Pia Waziri Mkuu Majaliwa amesema Tanzania inakkaribisha wawekezaji kutoka nchini Ubelgiji na mataifa mengine kuja kuwekeza katika Sekta za Viwanda, Nishati na Miundombinu.Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema hali ya siasa visiwani Zanzibar ni ya utulivu na Rais Dk. Ali Mohamed Shein anafanya kazi vizuri kwa kushirikiana na vyama vya upinzani.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mhe. Reynders aliyetaka kujua hali ya kisiasa inavyoendelea visiwani huko.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
06 Juni, 2016 .

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )