Saturday, July 9, 2016

Kodi ya Utalii Tanzania Yashtua mataifa Ulaya

Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye shughuli za utalii iliyoanza mwezi huu, imezishtua nchi 30 za Ulaya ambazo zimeiandikia barua Serikali ya Tanzania zikiomba ifikirie upya au isianze kutumika hadi mwaka ujao. 

Kodi hiyo, ambayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kukusanya mapato ili kuondokana na utegemezi, ilitangazwa kwenye Bunge la Bajeti lililopita na tayari Sheria ya Fedha imeshapitishwa kubariki matumizi yake, licha ya wabunge kuipinga kwa maelezo kuwa itazipa nchi washindani mwanya wa kukuza utalii. 

Dk Philip Mpango alisema walipata wazo la kuanzisha kodi hiyo kutoka nchi jirani ya Kenya, lakini wakati akitangaza hayo waziri mwenzake wa nchi hiyo alitangaza kuiondoa baada ya utalii kuathirika kutokana na mashambulizi ya kigaidi.

Wakati sheria hiyo ikianza kutumika nchini, nchi hizo za Ulaya ambazo ni wadau wakuu katika sekta ya utalii zimemwandikia barua hiyo Dk Mpango, naibu wake, Dk Ashatu Kijaji na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Chama cha Kitaifa wa Mawakala wa Usafiri na Wasimamizi wa Utalii (ECTAA) kutoka nchi 30 za Ulaya ndicho kinachoziwakilisha kampuni zaidi ya 70,000 za utalii barani humo. Nchi hizo ndizo zinazotoa asilimia 50 ya watalii wote duniani.

Katika barua yao iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa ECTAA, Michel de Blust, nchi hizo zilieleza wasiwasi wao kutokana na utambulishwaji wa ghafla wa kodi hiyo katika huduma za utalii, zikisema uamuzi huo unaongeza gharama za safari nchini.

“Najua utakubaliana na mimi kuwa kodi ina umuhimu wake na ina madhumuni yake, lakini inaweza kubadili mawazo ya watalii na wakachagua maeneo mengine,” inasema barua ya Blust.

Waziri wa Fedha na Mipango, “Mfano mzuri ni Kenya, utambulishaji wa kodi katika huduma za utalii mwaka jana ulishusha idadi ya watalii kwa asilimia nne na baadaye Kenya waliamua kuachana na kodi hiyo ili kudumisha ushindani wake.”

Barua hiyo inasema kodi hiyo katika huduma za utalii itaathiri waandaaji wa safari za watalii wanaotoa huduma nchini kwa sababu hakukuwa na tangazo la kuwaandaa kabla ya kuanzishwa kwa tozo hiyo.

“Waandaaji wa safari wa Ulaya wanawajibika na sheria inayomlinda mteja, hivyo wanatakiwa wawe wanafahamu bei na kodi mpya kabla. Kwa sasa ni vigumu mno kwa waandaji kubadili bei zao ghafla,” inasema barua hiyo.

Kadhalika, barua hiyo inaeleza kuwa Wakala wa Utalii wa Tanzania uliwasiliana na Wakala wa Ulaya kuhusu kodi hiyo na mawakala wa Ulaya wanatafakari kama wanaweza kuingia gharama hiyo au kujiondoa katika mpango huo.

Kama kodi hii ikiahirishwa, basi waandaaji wa safari za watalii watajipanga kuingia gharama hizi na kubadili mfumo wote wa huduma hizo Ulaya,” inasema barua hiyo.

Hivi karibuni, Waziri Maghembe alinukuliwa kwenye mkutano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), akisema kuwa Serikali haitabadili msimamo huo.

Alisema Sh7 bilioni wanazotarajia kupata kwa kutoza VAT kwenye huduma za utalii, zitawapa uwezo wa kutangaza utalii nje ya nchi na kuziba pengo la bajeti linalotokana na kushuka kwa utalii wa uwindaji. Alisema VAT itakayokatwa ni asilimia 18 ya kitu kilichonunuliwa na inatozwa wakati wa kununua huduma ya utalii.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema hajaiona barua ya ECTAA, lakini akasema watafanya kikao na Chama cha Wafanyabiashara za Utalii Tanzania (Tato) ili kujadili nini kifanyike ili sekta ya utalii isiyumbe.

“Hili ni suala mtambuka na hii VAT ilipitishwa na kikao cha bajeti, wizara kwa sasa haina la kufanya zaidi ya kutafuta njia mbadala ili sekta isiyumbe,” alisema.

Tovuti kwa ajili ya watalii ya Afrika, Safaribookings.com imeeleza kuwa wamekuwa wakipata barua pepe kutoka kwa wateja ambao wamepewa taarifa kutoka kwa wasimamizi wa watalii kulipa fedha za ziada.

Marc Harris, mkurugenzi wa kampuni ya Tanzania Odyssey inayotoa huduma za kitalii na yenye makazi yake nchini, aliliambia gazeti la Daily Telegraph la Uingereza kuwa kodi mpya ni janga kubwa ambalo halikutarajiwa na wengi.

“Watanzania wanaweza kufanya chochote kuhusu kodi, lakini suala la muda ndiyo tatizo. Wametupa taarifa hizi Juni 23, wiki moja tu kabla ya kodi kuanza kutozwa,” alikaririwa na gazeti hilo.

Alisema gharama kubwa itaonekana kwenye malazi ambayo inaonekana kuongezeka kwa asilimia saba.

“Kinachoshangaza ni kuwa Hifadhi za Taifa hazijasajiliwa VAT, lakini inatoza fedha hizo. Sijui watazitumiaje,” alisema Harris.

Mmiliki wa kampuni ya kitalii ya Safaribooking.com, Wouter Vergeer alisema muda mfupi waliopewa umewashtua.

“Maelfu ya wateja wameshtushwa na chaji hizo ambazo hazikutarajiwa. Wengi hawajapata muda wa kujipanga kwa tozo hizo, hata risiti zenyewe za VAT hatuna,”alisema.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )