Thursday, July 14, 2016

Mbunge wa Afrika Mashari Auawa Kikatili Burundi

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka nchini Burundi, Hafsa Mossi, ameuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa Bujumbura.

Mossi aliyewahi kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki katika serikali ya nchi hiyo, aliuawa jana katika barabara ya Gihosha eneo la Nyankoni.

Taarifa zilizothibitishwa na Msemaji wa Polisi wa nchi hiyo, Pierre Nkurikiye zilisema kuwa mauaji hayo yalifanyika saa 4:00 asubuhi. Nkurikiye alisema mbunge huyo alipigwa risasi kifuani kwenye moyo na kukimbizwa katika Hospitali ya Jeshi ya Kamenge ambako baadaye alipoteza maisha.

EALA ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambacho wanachama wake ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, ukiwa ni umoja wa kikanda wenye ushirikiano wa kibiashara huku ukikusudia kuwa na sarafu moja na shirikisho moja la kisiasa.

Mkazi wa eneo alikouawa Mbunge huyo, Achel Majabuka alisema kuwa alisikia mlio wa risasi na baadaye kuona watu wawili wakiondoka katika gari baada ya kuwatishia kwa silaha wakazi wa eneo hilo.

Kwa upande wake, Bunge la Afrika Mashariki katika taarifa yake iliyotolewa Kampala nchini Uganda, ilisema kuwa Mossi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Wabunge wa Burundi katika EALA, alipigwa risasi katika eneo la Mulanga Mashariki mwa Bujumbura.

Alimkariri msemaji huyo wa Polisi akieleza kuwa Mossi aliuawa karibu na nyumbani kwake, huku Mbunge mwingine wa Burundi katika EALA, Emerence Bucumi akithibitisha kifo hicho.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Kidega alilaani mauaji hayo na kumuelezea Mossi kuwa ni mchapakazi aliyekuwa amejikita kusimamia na kutetea utengamano wa ukanda huo.

Spika huyo ambaye yuko Uganda kwa ziara ya kikazi, ameishauri Serikali ya Burundi kuwatia nguvuni mara moja wauaji wa Mossi ambaye pia aliwahi kuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

“Ninatoa salamu za rambirambi kwa serikali, familia, marafiki na wananchi wa Burundi. Ninawaomba wawe watulivu katika wakati huu mgumu na ninaamini mamlaka husika zitafanya kazi kwa haraka kuhakikisha waliohusika na tukio hilo la kinyama wanatiwa nguvuni mara moja,” alisema Spika Kidega.

Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza alikielezea kifo cha mwanasiasa huyo kuwa ni cha kudharauliwa kwa serikali yake. Naye Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko, alisema amesikitishwa na kifo hicho cha Mbunge huyo aliyeeleza alikuwa rafiki na dada na kuwa jumuiya imepoteza mwakilishi aliyekuwa akifanya kazi bila kuchoka.

Mwaka jana, Mossi alitembelea wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda na kulia, ameuawa wakati mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi yakiwa yanaendelea kufanyika jijini Arusha.

Alikuwa na Shahada ya Uandishi wa Habari na aliwahi kufanya kazi katika BBC na alikuwa Waziri wa Burundi wa Masuala ya Afrika Mashariki hadi Juni 2012 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa EALA.

Pia, aliwahi Waziri wa Mawasiliano, Habari, Mahusiano na Bunge na Msemaji wa Serikali ya Burundi kuanzia mwaka 2005 hadi 2007.

Burundi, taifa katika Afrika Mashariki imekumbwa na ghasia na vifo kwa zaidi ya mwaka sasa.

Mgogoro huo wenye kuendana na umwagaji damu, umesababisha watu 1,500 kuuawa, huku ukiwahusisha wafuasi wa Rais Nkurunziza na wale wanaopinga ushindi wake wa uchaguzi wa Julai, 2015 kwa mara ya tatu, wakidai kuwa ulikiuka Katiba ya nchi hiyo.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )