Monday, July 4, 2016

Mjamzito ajifungulia kwenye korido Baada ya Wauguzi Kugoma Kumsaidia

Mjamzito mmoja, Magreth Charles (22), mkazi wa Kata ya Lyabukande Wilaya ya Shinyanga amejifungulia kwenye korido la Kituo cha Afya cha Lyabukande baada ya kukosa huduma kutoka kwa wauguzi.

Mjamzito huyo alilazimika kujifungulia kwenye korido kutokana na wauguzi katika kituo hicho kugoma kutoa msaada wakidai wako kwenye mapumziko na kumtaka aende sehemu nyingine.

Mama mkwe wa mjamzito huyo, Rachel Mpanda alisema walifika kituoni hapo wakitokea kijiji cha Kizungu jirani na kituo hicho na walielezwa na mtu waliyemkuta kuwa wauguzi wako mapumzikoni, hivyo hakutakuwa na huduma yeyote.

“Baada ya muda kidogo tukiwa tunatafuta namna ya kwenda kituo kingine, mwari wangu alianza kusukuma mtoto, hivyo nikaamua kuomba msaada kwa wapitanjia ili wamsaidie ajifungue, alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume,” alisema Mpanda.

Diwani wa kata hiyo, Joseph Misiri alisema tukio la mwanamke huyo kujifungua kwenye korido si la kwanza na kwamba kuna mwanamke mwingine alikosa huduma hiyo na kusababisha mtoto kufariki dunia.

“Serikali haina budi kuwachukulia hatua wauguzi katika kituo hiki kwani wanasababisha kupoteza maisha ya watoto wachanga, mwishowe watasababisha kupoteza maisha kwa wajawazito kwa kukosa huduma ya matibabu,” alisema Misiri.

Mmoja wa wauguzi katika kituo hicho, Zulfa Mussa alisema kituo hicho kina watumishi watatu; muuguzi mmoja alikuwa amempeleka mgonjwa hospitali ya rufaa, daktari mfawidhi wa kituo, Kadela Mashaka alikuwa semina na yeye alikuwa zamu usiku, hivyo alitakiwa kupumika mchana huo.

“Kwa kawaida aliyekuwa zamu ya usiku anatakiwa kwenda kupumzika kujiandaa na zamu yake nyingine, hivyo niliondoka kituoni na kumwacha mtaalamu wa maabara,” alisema Zulfa.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba alipohojiwa alisema hana taarifa na kuahidi kufuatilia.


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )