Thursday, July 7, 2016

Serikali Yaingilia kati Sakata la Mama Aliyejifungua Watoto Watatu Muhimbili Na Kisha Kuzuiliwa Kutoka Baada Kushindwa Kulipia Gharama

Mzazi aliyejifungua watoto watatu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini akazuiwa wodini kutokana na kudaiwa gharama za matibabu, jana aliruhusiwa kuondoka baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuingilia kati suala hilo.

Mzazi huyo, Stella Nnko (38) aliyefikishwa Muhimbili kwa rufaa akitokea Hospitali ya Mnazi Mmoja, alikuwa akidaiwa Sh540,595.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ndiye aliyeingilia kati suala hilo na kuagiza mama huyo apewe watoto wake na kuruhusiwa ambapo  jana asubuhi katibu mkuu wa wizara, Dk Mpoki Ulisubisya alimtembelea mzazi huyo kabla ya kuondoka hospitalini hapo.

Akizungumzia tukio hilo, Stella alimshukuru Waziri kwa kuingilia kati suala hilo na kuwaomba wasamaria wema kumsaidia katika matunzo ya watoto hao kwa kuwa uwezo wake kiuchumi si mzuri.

Alisema hajawahi kuonana na baba wa watoto hao tangu alipompa ujauzito, na yeye hana uwezo wa kuwatunza.

“Ninayaendesha maisha yangu kwa kukaanga mihogo, shughuli ambayo kwa sasa nitashindwa kuendelea kuifanya kwa sababu ya kuwahudumia hawa watoto,” alisema Nnko.

“Nyumbani nimemwacha mwanangu wa miaka miwili na nusu na sina msaidizi wala ndugu.”

Stella anaishi Kivule, Ilala jijini Dar es Salaam. Kabla ya kuondoka Muhimbili, watoto hao watatu walipewa chanjo ya kupooza, BCG ya kifua kikuu na matone ya vitamin A.

Mtoto mmoja kati yao ni wa kiume na alizaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 2.8 wakati wa kike wawili walikuwa na uzito wa kilo 2.5 na 2.1.

Akizungumzia sakata hilo, mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha MNH, Aminiel Aligaesha alisema Stella alifikishwa hospitalini hapo Juni 29 mwaka huu kwa dharura akitokea Mnazi Mmoja na kufanyiwa upasuaji Juni 30.

Lakini alikanusha taarifa kwamba MNH ilimzuia kutoka, bali alipewa hati ya malipo ili ajiandae kulipa, kinyume na kauli ya Stella kwamba aliruhusiwa kuondoka na kupewa hati ya malipo na alipoeleza kuwa hana uwezo, alizuiwa mpaka atakapochangia huduma.

“Wakati Stella akipewa huduma na kusubiri kuruhusiwa, alipelekewa gharama ya jumla ya Sh477,131 ikiwa ni gharama ya kujifungua kwa upasuaji na huduma zote alizozipata tangu alipopokelewa, zikiwemo dawa na vitendanishi. Hakuzuiwa, ila alipewa hati ya malipo ili ajiandae kulipa,” alisema Aligaesha.

Alisema pamoja na hayo, Nnko amesamahewa kulipa gharama zote za matibabu na tayari amesharuhusiwa kwenda nyumbani.

Kuhusu suala la tozo kwa mama wajawazito, Aligaesha alisema ni utaratibu ambao uliwekwa na hospitali wa kuchangia huduma kwa kuwa tangu wameanza mfumo huo dawa na vitendanishi vimekuwa haviadimiki ikilinganishwa na hapo awali.

“Dhamira yetu ni kuhakikisha kila mgonjwa anayekuja kutibiwa MNH anapata dawa na huduma zote kwa gharama nafuu. Tunawaomba wananchi kuchangia huduma zote za afya ili tuweze kupata fedha na kutoa huduma kwa mfumo endelevu.Ndiyo maana ndani kuna duka la MSD,” alisema

Alisema iwapo akitokea mgonjwa hana uwezo wa kuchangia huduma, utaratibu wa kumuombea msamaha unatumika na atapata huduma bila malipo.

Maiti iliyozuiliwa
MNH pia ilidaiwa kuzuia mwili wa marehemu Hilda Mbawala aliyefariki Juni 26 kutokana na ndugu zake kushindwa kulipia gharama za Sh1.4 milioni, lakini Aligaesha alikanusha madai hayo.

“Wakati marehemu akitibiwa, ndugu walikuwa wanapewa taarifa na mwenendo wa matibabu ya ndugu yao, ikiwamo kuhimizwa kuchangia huduma,” alisema Aligaesha.

“Baada ya kifo hicho, ndugu wa marehemu walipewa hati ya gharama ya matibabu ya Sh1.4 milioni ili wakajipange jinsi ya kulipa.”

Alisema ndugu hao walisema hawana uwezo wa kulipia kiasi hicho cha fedha na Juni 30 waliwasiliana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii ili wasaidiwe na baada ya majadiliano pande zote mbili zilikubaliana kuwa walipe Sh800,000.

“Wakati makubaliano hayo yakiwa kwenye hatua za kuidhinishwa na mamlaka husika, ndipo ndugu walipokimbilia kwenye vyombo vya habari na kulalamika kuwa hospitali imezuia mwili.

"Ukweli ni kwamba wamelipa kiasi hicho cha Sh800,000 na wamesamehewa deni la Sh 623,747.64 na mwili waliuchukua Julai 5,” alisema.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )