Tuesday, July 5, 2016

Taasisi ya Maridhiano kutafuta muafaka kati ya UKAWA na Naibu Spika


TAASISI ya Maridhiano inatarajia kuwasilisha ujumbe kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kuomba kuyakutanisha makundi mawili yanayosigana bungeni ili kuleta muafaka wenye tija kwa taifa.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sheikh Sadick Godigodi jana alisema kumeguka kwa Bunge kunakosababishwa na Kambi ya Upinzani kuona inaonewa na maamuzi ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson kunahitaji viongozi wa dini kuingilia kati na kupata suluhu.
 
"Tunatarajia katika Bunge lijalo litakaloanza Septemba kuwasilisha ujumbe kwa Spika ili tupewe nafasi ya kutatua mgogoro huu kwa maana wabunge wote wanatakiwa kuwepo bungeni kuwakilisha matatizo ya wananchi," alisema Sheikh Godigodi.
 
"Haiwezekani kundi moja likawa nje na jingine likaendelea, tunahitaji maridhiano ya pande zote mbili za muhimili huo.”
 
Kambi ya Upinzani Bungeni ilisusia vikao vya Bunge la Bajeti kwa zaidi ya siku 70 kupinga kile kilichoita kuburuzwa na
Naibu Spika katika uendeshaji wa chombo hicho cha kutunga sheria.
 
Kambi hiyo, ilianza kutoka nje Mei 30 baada ya Naibu Sika kukataa hoja ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari (Chadema), ya kutaka Bunge likatize shughuli zake na kujadili hoja ya kufukuzwa kwa wanafunzi zaidi ya 700 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
 
Ingawa kitendo hicho cha Naibu Spika kiliwaudhi wabunge wa chama tawala (CCM) na Upinzani, kambi hiyo haikurudi ndani mpaka Bunge lilipoahirishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katikati ya wiki iliyopita.
 
Mshauri wa mambo ya kisheria na kidiplomasia wa taasisi hiyo ya Maridhiano, Agustino Matefu alisema mbali na kusuluhisha migogoro chochezi ya kidini kwa kutoa elimu sahihi kwa umma, pia wamejikita katika kusuluhisha migogoro sugu kati ya wakulima na wafugaji nchini.
 
“Tumetoa mchango mkubwa wa kuleta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima mkoani Morogoro katika wilaya za Mvomero, Kilombero na Kilosa (na) ndio maana watanzania wanaona hali ni kama sasa imekuwa shwari,” alisema Matefu.
 
Matefu alisema wamepata mualiko rasmi kwa uongozi wa Mkoa wa Iringa na wanatarajia kwenda huko baada ya uzinduzi rasmi wa taasisi hiyo utakaofanyika Julai 13 jijini Dar es Salaam.
 
Katibu wa taasisi hiyo, Mchungaji Oswald Mlay alisema kuwa uzinduzi na utambulisho wa taasisi hiyo utaendana na utoaji tuzo ya amani kwa viongozi na watu mbalimbali waliojitoa kuhamasisha udumishwaji wa amani nchini.
 
Wanaotarajiwa kupewa tuzo ni Mama Maria Nyerere kwa niaba ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambae atatunukiwa tuzo ya Amani uasisi wa amani ya taifa.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )