Thursday, September 22, 2016

Rais Magufuli Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Balozi Wa Urusi Na Jamhuri Ya Korea Hapa Nchini .....Azungumzia Ujenzi wa Daraja la Salender

Ujenzi wa Daraja la Salender litakalounganisha eneo la Coco Beach na eneo Agha Khan kupitia baharini Jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuanza Mwezi Juni Mwakani baada ya Serikali ya Tanzania kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa fedha za ujenzi kutoka benki ya Exim ya Korea.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Septemba, 2016 muda mfupi baada ya kufanya Mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa kilometa 7 zikiwemo kilometa 1.4 zitakazopita baharini, unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 na daraja hilo litasaidia kupunguza adha ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

"Mchakato wa kulijenga hili daraja la Salender unaendelea vizuri kwa sababu hivi sasa kampuni ya Kikorea ambayo inafanya usanifu ipo kwenye hatua za mwisho na zabuni zinategemewa kutangazwa mwezi wa tatu Mwaka kesho na zitakwenda haraka, kwa hiyo mambo yakienda vizuri ujenzi unaweza kuanza mwezi wa sita, bahati nzuri fedha zote zipo na zimeshatolewa na Benki ya Exim ya Korea" Amesema Rais Magufuli.

Aidha, Dkt. Magufuli amemshukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa juhudi alizozifanya zilizowezesha kujengwa kwa hospitali ya Mloganzila  kwa ufadhili wa Jamhuri ya Korea na kwamba hospitali hiyo itakuwa ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu na kwamba tayari Madaktari na Wataalamu takribani 100 waliopata mafunzo nchini Korea na wenye ujuzi wa namna ya kutumia teknolojia inayowekwa kwenye hospitali hiyo wapo hapa nchini.

Rais Magufuli ambaye ameelezea nia ya Serikali ya Tanzania kufungua ofisi za Ubalozi Mjini Seoul nchini Korea ameongeza kuwa Serikali yake imedhamiria kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi kwa lengo la kuwaletea manufaa wananchi ikiwemo kutumia teknolojia na ujuzi wa nchi ya Korea katika ujenzi wa Meli.

Kwa upande wake, Balozi wa Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young ametoa salamu za pole kufuatia maafa ya tetemeko la Ardhi yaliyotokea Mkoani Kagera na mikoa jirani, na ameahidi kuwa Korea itatuma timu ya wataalamu kuja kuona namna ya kusaidia.

Balozi Song Geum-Young pia amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Korea itaendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kwamba itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa Daraja la Salender, Meli, Hospitali ya Mloganzila na mingineyo.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa Urusi hapa nchini Mhe. Yuri Popov ambapo viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo huku wakitilia mkazo katika kukuza biashara na uwekezaji.

Pamoja na hayo Balozi Yuri Popov amepongeza na kuelezea kufurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli katika kuimarisha uchumi huku akibainisha kuwa kwa hatua hizi anaamini ajenda ya kujenga uchumi wa viwanda itafanikiwa.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea taarifa ya hali ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na katika mazungumzo yake na Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele, amemtaka kuendelea kuimarisha utendaji kazi wa maabara hiyo ili kuongeza ufanisi wa majukumu yake ambayo ni kufanyia uchunguzi vielelezo vya makosa ya Jinai na usimamizi wa sheria za udhibiti wa kemikali na udhibiti wa vinasaba vya binadamu (DNA).

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

22 Septemba, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na kumkaribisha  Balozi wa Urusi hapa nchini Yuri Popov aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkemia Mkuu wa Serikali Profesa Samwel Manyele Ikulu jijini Dar es Salaam.
PICHA NA IKULU.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )