Monday, October 3, 2016

SIKIKA Yaitaka Serikali Iache Siasa Upatikanaji wa Dawa.....Yatoa Mapendekezo 6 Kutatua Tatizo

Wiki iliyopita Sikika ilikutana na vyombo vya habari kujadili uhaba wa dawa unaoikabili Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Vyombo vya habari kwa nyakati tofauti vilitoa taarifa sahihi kuhusu tatizo hili.

Hata hivyo, majibu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Bohari Kuu ya Dawa hayakuonesha kutoa kipaumbele kwa tatizo hili. Kwa kuwa taarifa za uhaba wa dawa zilipatikana kutoka kwenye tovuti ya Bohari Kuu ya Dawa, tulitegemea majibu yenye ukweli,weledi na kuonesha ukubwa wa tatizo kutoka kwa wahusika. Taarifa hizo zingesaidia Ofisi ya Rais kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuona uharaka na umuhimu wa kutatua tatizo hili ili kuwasaidia wananchi kwa wakati. Badala yake majibu ya Wizara na Bohari Kuu yalipoteza msingi wa tatizo kama ifuatavyo;

(i)  Vyombo vya habari vilitumia takwimu kutoka katika tovuti rasmi ya Bohari Kuu ya Dawa kwamba kuna upungufu wa asilimia 47 ya aina mbalimbali za dawa zilizotakiwa kuwepo kwenye orodha ya dawa MSD. Tarehe 27 Septemba 2016, Wizara ya Afya ilikanusha kwa kudai kwamba aina ya dawa zilizokuwepo ni asilimia 53. Hata hivyo, mtu akisema uhaba ni asilimia 47 ya aina ya dawa na mwingine akasema uwepo ni asilimia 53 wote wanamaanisha kitu kile kile.

(ii) Taarifa za vyombo vya habari zilionesha uhaba wa baadhi ya dawa muhimu ambazo zilitarajiwa kupatikana MSD muda wote Taarifa hizi zilikusudia kuonesha mifano ya kiwango cha ukubwa wa upungufu wa dawa. Badala ya kujibu hoja ya msingi, yaani upungufu wa dawa nchini kwa ujumla; Wizara iliamua kujikita kwenye kutaja uwepo wa baadhi ya dawa kama vidonge vya paracetamol na zingine chache.

(iii) Bohari Kuu ya Dawa ilinukuliwa na vyombo vya habari ikikanusha uwepo wa upungufu wa dawa na kusema kwamba serikali imefanya maajabu kwa kuipatia MSD jumla ya Shilingi bilioni 20 kwa robo ya 2016/2017. Hata hivyo, bilioni 20 ni pungufu ya kiwango halisi ambacho kingehitajika (Shilingi bilioni 62.5), kwa robo ya kwanza ya mwaka iwapo bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 251 ingegawanya sawa na kutolewa katika awamu nne. Je, Bohari Kuu ya Dawa inaposema serikali imefanya maajabu ina maana haihitaji fedha zaidi kwa ajili ya kutatua tatizo la dawa nchini?

(iv) Wizara ya Afya imeahidi kuongeza akiba ya baadhi ya dawa kuanzia mwezi Oktoba, 2016. Hii ni sawa na kukiri kwamba kulikuwa na upungufu wa dawa. Ingawa tunaipongeza wizara kwa hili, Wizara haikueleza ni lini itapata fedha zilizobaki na iwapo ongezeko hilo la dawa litakidhi mahitaji halisi.

Katika kufafanua suala hili, Sikika ingependa kuelezea umma na wadau wa sekta ya afya ukweli kuhusu upungufu huu sugu wa dawa na vifaatiba kwenye Bohari Kuu ya Dawa na katika vituo vya kutolea huduma za afya:

(i)  Uhaba wa dawa na vifaa tiba katika Bohari Kuu ya Dawa siyo tatizo jipya, bali ni la muda mrefu, ambalo serikali yenyewe imekuwa ikikiri kupitia taarifa zake mbali mbali. Isipokuwa sasa limefikia kiwango kikubwa, hata kupelekea uhaba wa dawa kama za chanjo kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu.
(ii) Kila mwaka, Wizara ya Afya wamekuwa wakiahidi Bungeni kutatua upungufu na uhaba wa dawa muhimu na vifaatiba. Pia Wizara ya Afya imekuwa ikiahidi bungeni kila mwaka kulipa deni inalodaiwa na MSD ili kuboresha ufanisi wa bohari. Hata hivyo uhaba wa dawa umeendelea kuwepo na deni la MSD limekuwa likikua kila mwaka.

(iii) Uhaba ukitokea MSD moja kwa moja unaathiri upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma, kwa sababu mfumo wa sasa unalazimisha vituo kuagiza dawa kutoka MSD kwanza kabla ya kuruhusiwa kununua mahali pengine. Pamoja na hilo, mgao wa fedha za dawa kwa vituo hivyo hupelekwa moja kwa moja MSD ambapo vituo haviwezi kuzichukua kuagiza dawa pengine pale wanapokosa dawa MSD.

(iv) Mnamo Septemba 16, 2016, tovuti ya MSD ilionesha ukosefu wa asilimia 47 wa aina mbali mbali za dawa. Miongoni mwa dawa na vifaatiba vilivyokosekana ni vile vinavyotumika katika matibabu muhimu ya kupunguza vifo, mfano dawa za kuharisha kwa watoto (ORS+Zinc), vifaa vya kujifungulia (Delivery kits), dawa za maumivu, dawa za magonjwa ya moyo na chanjo kama vile za surua, homa ya manjano na kichaa cha mbwa.

(v)  Mojawapo ya sababu za uhaba huu ni serikali kushindwa kutenga na kutoa fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya nchi ya dawa muhimu na vifaatiba. Kwa mfano, mahitaji ya sasa ya dawa na vifaatiba ni zaidi ya shilingi bilioni 577 lakini bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu ni shilingi bilioni 251, ambapo kati ya hizo, shilingi bilioni 108 ni za kulipa deni la MSD.

(vi)  Vituo vya afya vya umma vinapata usumbufu mkubwa kutokana na utaratibu unaovilazimisha kutuma maombi ya dawa MSD licha ya kufahamu ukweli kwamba hazipo. Baada ya vituo kupata uthibitisho wa maandishi wa kutokuwepo dawa MSD, ndipo vinaruhusiwa kufanya taratibu zingine. Pamoja na usumbufu huu, baadhi ya vituo vimemudu kukabiliana na uhaba wa dawa kwa kutumia vyanzo mbadala vya fedha kununua dawa kutoka kwa wauzaji binafsi. Mfano halisi ni katika vituo vya afya vya wilaya za Kondoa na Kilolo ambapo Sikika ilifuatilia kwa kina.

Kutokana na uzoefu wa Sikika wa kufanya kazi katika sekta ya afya kwa takribani miaka kumi, tunashauri mapendekezo yafuatayo yafanyiwe kazi:
(i)  Bohari Kuu ya Dawa iachwe iwe taasisi au kampuni huru itakayofanya maamuzi yake yenyewe na kukusanya mtaji kushindana na wauzaji wengine binafsi wa dawa nchini.
(ii) Serikali ifute ulazima wa vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kuagiza dawa MSD kwanza, badala yake viachwe huru kuamua kununua kutoka kwa muuzaji yeyote mwenye dawa ambaye anadhibitiwa na kuhakikiwa na serikali.

(iii) Serikali ihakikishe kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya dawa muhimu na vifaatiba zinapelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za vituo au Halmashauri badala ya utaratibu wa sasa ambapo zinapelekwa kwenye akaunti za vituo zilizopo MSD.

(iv) TAMISEMI iimarishe na kusimamia uwezo wa vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri ili kujiendesha vyenyewe, na Wizara ya Afya ijikite katika kusimamia ubora na udhibiti wa bei za dawa.

(v)  Tunaomba watendaji na viongozi katika sekta ya Afya wafanye kazi kitaalam zaidi badala ya kisiasa.
(vi) Mwisho, wakati Wizara ya Afya ikifanyia kazi mapendekezo haya. tunaiomba Ofisi ya Rais kuagiza fedha zitolewe kama mpango wa dharura kutatua tatizo lililopo la dawa, ikiwa ni pamoja na kulipa deni lote la MSD.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )