Sunday, January 22, 2017

Tanzania Kujifunza Toka China Kuhusu Namna ya Kukuza Uchumi

Serikali imesema iko tayari kujifunza namna ambavyo China imefanikiwa katika kukuza uchumi wake, ili kutengeza mfumo utakaoleta maisha bora kwa Watanzania wote.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua sherehe za Mwaka Mpya wa China, ambao kwa mwaka huu unajulikjana kama ‘Mwaka wa Jogoo” katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Samia alisema mafanikio ya China katika kuwatoa wananchi wake katika umasikini, unaendelea kuihamasisha Serikali na hasa katika kipindi hiki ambacho inaongia katika mageuzi ya kiuchumi.

“Tunaridhishwa jitihada zenu katika kumaliza tatizo la rushwa, tunafahamu mabadiliko mliyofanya ndio yametoa matokeo ya usimamizi mzuri wa uchumi. Najua mabadiliko yanaweza kuwa ajenda ya malengo yetu, lakini kuna sababu nzuri kwa sisi kuwa na nia.”

“China imeweza katika siku za nyuma, sisi pia tunaweza kufanya sasa, lakini tunahitaji kuungwa mkono,” alisema Samia.

Aidha, alisema uhusiano kati ya China na Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba wanathamini mchango mkubwa wa China katika maendeleo ya Tanzania.

Akizungumzia nyanja ya kisiasa, alisema ubadilishanaji uzoefu baina ya nchi hizo mbili hasa katika masuala ya utawala, umeongezeka na kuzaa matunda.

Alisema ziara ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, ilikuwa si tu kwajili ya kuboresha mahusiano ya kidiplomasia pekee, bali pia kufanya kazi ya kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na mikakati ya miradi ya miundombinu, ambayo ni muhimu katika kusaidia maendeleo ya viwanda nchini.

Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema sikukuu hiyo muhimu, wamefanya hivyo ili kuruhusu Watanzania kujua utamaduni wa Wachina, huku akitoa shukrani kwa Serikali kwa msaada na ushirikiano.

Alisema, mwaka uliopita ulikuwa ni muhimu kwa ajili ya mahusiano ya China na Tanzania na pia ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa matokeo ya Mkutano wa FOCAC uliofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Alisema chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, Serikali ya Tanzania inasisitiza mapambano dhidi ya rushwa na uvivu, na kuhimiza uwajibikaji ili watu wote waweze kunufaika.

Alisema kwamba Rais Magufuli alianza kwa kuchukua hatua madhubuti za mfululizo, kukomesha matatizo hayo. Balozi Youqing alisema Rais Magufuli alimuandika barua Rais wa China, Xi Jingping na watu wa China, kumpongeza kwa mafanikio ya Serikali ya China iliyopata katika mapambano ya rushwa na kufanya mageuzi ya kina.

“Alisifu uhusiano wa kindugu kati ya Tanzania na China, alisisitiza kwamba ushirikiano wa Tanzania na China, na mpango wa “Belt and Road” utasaidia maendeleo ya viwanda nchini Tanzania na alisema Tanzania itaendelea kuinga mkono China katika masuala mbalimbali,” alisema Balozi Youqing.

Aliongeza kuwa China inafurahia ushirikiano wa kina katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kimataifa. Kwamba katika uwanja wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, China imekuwa mkandarasi mkubwa na chanzo cha pili kwa uwekezaji. Alitaja baadhi ya miradi mikubwa ni reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Bandari ya Bagamoyo na hifadhi ya viwanda Buguruni; na mradi wa biashara ya muhogo pia uko kwenye ukuaji mzuri.

Alisema Ubalozi wa china nchini utatekeleza kikamilifu makubaliano ya mawaziri wawili ambao ni Wang Yi wa China na Dk Augustine Mahiga wa Tanzania ili kuendeleza mahusiano kwa manufaa ya nchi hizo mbili. Balozi huyo pia alisema ubalozi wake, umechangia Sh milioni 100 katika Mfuko wa Maendeleo ya Serikali, ili kusaidia sekta ya elimu nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema Tanzania imepewa kipaumbele cha kipekee katika nchi za Afrika, kwakuwa China imetoa dola za Mareakni milioni 60 kwa ajili ya kusaidia nchi za Afrika na imechagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kati ya nne, ambazo ni Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya.

Alisema kama ulivyo mwaka huo wa Jogoo, mahusiano ya China na Tanzania nayo yanazidi kuwika katika nyanja mbalimbali. “…Katika hili la viwanda China imeahidi kama sisi tutachangamkia fursa hizo, viwanda vingi vidogovidogo na vile ambavyo sasa hivi vinachukua ajira ya watu wachache, kwasababu wao wanajikita katika teknolojia kubwa, viwanda hivyo vitahamia Tanzania,” alisema Dk Mahiga.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )