Sunday, January 22, 2017

Waumini Kanisa la Anglikan Wamzuia Askofu Mokiwa kufanya vikao

Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa la Anglikana, Dk valentino Mokiwa jana alishindwa kuendesha vikao viwili baada ya kundi la waumini kufika Usharika wa Ilala kwa lengo la kuzuia.

Askofu Mokiwa, ambaye anapinga uamuzi wa Askofu Mkuu wa Anglikana, Dk Jacob Chimeledya kumvua madaraka kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, alikuwa aendeshe vikao vya kamati ya fedha na halmashauri kuu, lakini alilazimika kuviahirisha baada ya kundi hilo kufika eneo hilo.

Wakati waumini hao wakizuia vikao hivyo kufanyika, mashemasi, mapadri, wainjilisti na waumini wa dayosisi hiyo wametoa tamko la kumuunga mkono Dk Mokiwa wakipinga uamuzi wa mkuu wa kanisa hilo kumvua madaraka.

Askofu Mokiwa anapinga uamuzi wa kumvua madaraka akisema hauwezi kufanywa na mkuu wa kanisa, bali na halmashauri kuu ya jimbo ambayo anasema haikushirikishwa zaidi ya kutaarifiwa uamuzi huo.

Tukio la jana la kumzuia Dk Mokiwa kufanya mkutano lilitokea saa mbili asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Nicolau wilayani Ilala, ambako kuna ofisi ya Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam.

Mmoja wa watu walioshiriki kuzuia vikao hivyo, Haule Sylvester ambaye alijitambulisha kuwa kiongozi wa waumini wa Anglikana jijini Dar es Salaam, alisema walichukua uamuzi huo kwa kuwa Dk Mokiwa ameshavuliwa uaskofu.

“Huyu (Dk Mokiwa) hapaswi kufanya shughuli zozote za kanisa kwa sababu si askofu. Lakini amekuwa akiendesha vikao vya siri na mapadri wanaomuunga mkono,” alisema Sylvester.

“Jana (juzi) alifanya kikao cha siri. Leo (jana) alikuwa aongoze vikao viwili, kikiwamo cha bodi ya fedha ya dayosisi hii, ndiyo maana tumemzuia.”

Alifafanua kuwa baada ya kikao hicho cha fedha kilichokuwa kimepangwa kuanza saa 3:00 asubuhi, kikao ambacho kingefuata ni cha halmashauri kuu ya dayosisi ambacho kingefanya uamuzi wa mambo ambayo yangejadiliwa na bodi ya fedha.

Sylvester alisema kwa mujibu wa katiba ya dayosisi hiyo, vikao hivyo vyote vinatakiwa viongozwe na mwenyekiti ambaye ni askofu wa dayosisi.

Alisema halmashauri ina wajumbe 10 akiwamo askofu wa dayosisi, wakati kikao cha bodi ya fedha kina wajumbe zaidi ya 200 na kina lengo la kupanga bajeti ya mwaka.

“Ki utaratibu ili kuendesha vikao hivi, lazima uwe askofu wa jimbo la Dar es Salaam. Tunamsihi Mokiwa aache kufanya kazi na kutumia ofisi kwa kofia ya uaskofu,” alisema.

Alisema waumini wengi walipanga kushiriki katika mchakato huo, lakini walienda 20 baada ya kutoa taarifa polisi.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Yohana Sanga ambaye ni ofisa habari wa Dk Mokiwa alisema vikao hivyo vilikuwa vya kawaida vya dayosisi hiyo na vililenga kujadili maendeleo ya kanisa.

“Tulishangaa kuona kundi lile la watu, ambalo chimbuko lake limetoka Kanisa la Magomeni linalompinga Askofu Mokiwa,” alisema. 

Mbali na kundi hilo, kilichowasikitisha zaidi ni kuona magari sita ya polisi, wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), yaliyokuwa yameegeshwa nje ya kanisa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Ilala, Salum Hamduni alisema  kuwa askari hao walikuwa katika doria ya kawaida.

Sanga alisema baada ya kundi hilo kufika katika eneo hilo, liliingia moja kwa moja kanisani na walipowauliza walijibiwa kuwa wanakwenda kujadili masuala ya kanisa.

Alisema baada ya kuona hivyo, walisita kufungua ofisi iliyoandaliwa kwa ajili ya vikao na baada ya majadiliano ya muda mrefu, waliahirisha.

“Walivyoona hatufungui ofisi, waliamua kuondoka kwa mafungu.Lengo lao lilikuwa kuvunja vikao hivi,” alisema Sanga.

Taarifa ya viongozi hao wanaomuunga mkono Askofu Mokiwa, inasema bado wanaendelea kumtambua na kumuunga mkono kiongozi huyo kama askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na kwamba uamuzi uliochukuliwa dhidi yake ni batili.

Hivi karibuni, Askofu Mkuu, Chimeledya alimtaka Dk Mokiwa ajiuzulu kwa kile alichodai kuwa anatumia vibaya madaraka yake na ubadhirifu wa fedha.

Hata hivyo, Dk Mokiwa alikanusha madai hayo na kusema mgogoro wa kanisa hilo ni wa kutengenezwa na maadui zake.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )