Monday, February 13, 2017

Rais Magufuli Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Wageni Mbalimbali Ikulu Jijini Dar Es Salaam

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Daniel Kidega amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ya kujenga uchumi wa Tanzania na amewaomba wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki kuunga mkono mfano mzuri unaooneshwa na kiongozi huyo.

Mhe. Daniel Kidega amesema hayo leo tarehe 13 Februari, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na Mhe. Rais Magufuli na kufanya nae mazungumzo yaliyojikita kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi wanachama, kuinua hali ya uchumi na kutatua matatizo yanayozikabili baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya.

“Nikueleze kitu kimoja, Tanzania na Afrika Mashariki tumebahatika sana kupata kiongozi kama Rais Magufuli ambaye anatuongoza vizuri, analeta maendeleo na mabadiliko, naomba watu wote wa Tanzania na Afrika Mashariki wamuunge mkono, kwamba kiongozi kama yeye ndiye tunayemtaka, tuangalie viongozi wanaoleta maendeleo na mabadiliko kwa watu wetu ili tuwe vizuri” amesisitiza Mhe. Daniel Kidega.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke ambapo viongozi hao wamezungumzia namna Tanzania na Uingereza zitakavyoimarisha uhusiano na ushirikiano katika uwekezaji na biashara, mapambano dhidi ya Rushwa na dawa za kulevya, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha huduma za usafiri wa anga.

Kwa upande wake Mhe. Dkt. Magufuli amemshukuru Mhe. Sarah Cooke na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano wake wa kihistoria na Uingereza katika kujenga uchumi imara wa Tanzania, kupambana na rushwa na dawa za kulevya na amemshukuru Uingereza kuongeza fedha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali itakayosaidia maendeleo hapa nchini.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi Mpya wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bw. Bhaswar Mukhopadhyay ambapo viongozi hao wamezungumzia juu ya shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa kwa ushirikiano wa Tanzania na IMF.

Bw. Bhaswar Mukhopadhyay amempongeza Rais Magufuli kwa hatua kubwa na muhimu anazochukua kuimarisha uchumi, zilizowezesha kiwango kizuri cha ukuaji wa uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa.

Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Mhe. Balozi Liberat Mfumukeko.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

13 Februari, 2017
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )