Thursday, February 16, 2017

Waziri Mkuu: Hatutakubalina Na Wachochezi ...... Amani Kwanza, Masuala Mengine Baadaye

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitakubali kuona watu wachache wanachochea vurugu na kusababisha watu wengine wapoteze maisha ilhali wao hawadhuriki.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Februari 15, 2017) wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa mjini Kibaya, wilayani Kiteto, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku sita mkoani Manyara, alisema: “Hatutakubaliana na wachochezi. Hatutakubaliana na yeyote atakayesababisha kifo. Tukibaini kuna uchochezi, tutawasaka wahusika na kuwashughulikia,” alisema.

“Hapa kulikuwa na majina ya ajabuajabu, hatutakubali Kiteto iitwe Soweto au Kossovo, hapa ni Tanzania. Hatuwezi kuishi kwa kubaguana, ni lazima tuheshimu maamuzi ya wazee wetu wa kimila ambao wamesimamia zoezi hili ili kurejesha amani ya Kiteto,” alisema.
 
Alisema zamani Kiteto kulikuwa hakuna lugha ya amani lakini hali kwa sasa imebadilika na kuwa nzuri na akasisitiza kwamba hakuna kurudi nyuma.

Alisema anamshukuru Waziri Mkuu mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa kufuatilia suala hilo na kuunda tume ya kutafuta amani wilayani Kiteto. “Nilipoingia madarakani, nami nilianza kufuatilia suala hilo ili nijue chanzo hasa ni nini. Nikabaini kuwa mgogoro mzima umechangiwa na chokochoko tu za watu wachache,” alisema.

Mapema, viongozi wa kimila walimkabidhi Waziri Mkuu rungu, jembe dogo na jani la mti wa asili (Kimasai unaitwa elisibie) ikiwa ni ishara amani ya kukomesha mapigano baina ya wafugaji na wakulima. Pia alishiriki dua ya kuombea amani ambayo iliongozwa na viongozi wa dini.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )