Thursday, March 2, 2017

CCM yamjibu hivi Mjane wa Kapteni Komba kuhusu mafao ya mumewe

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Mjane wa Marehemu, Kapteni Komba, Bi. Salome Komba kufuatilia malipo ya mafao ya mumewe kwa uongozi wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT) ambako ndiko alikokuwa akifanyia kazi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo, ametoa maelekezo hayo ikiwa ni siku moja tu baada ya Salome kukaririwa  akimuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli aingilie kati kumsaidia ili alipwe mafao ya marehemu mume wake yanayofikia Shilingi Milioni 75.

Mpogolo amesema ofisi yao haiwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu masuala yanayohusu fedha yanapaswa kufafanuliwa vyema na uongozi wa kundi lao la TOT ambako Komba alikuwa akifanya kazi.

“Ofisi yao haiwezi kulizungumzia kwa sababu masuala yanayohusu fedha yanapaswa kufafanuliwa vyema na uongozi wa kundi lao la TOT ambako Komba alikuwa akifanya kazi,” amesema.

Kwa mujibu wa Bi. Salome, hadi sasa wakati mumewe akitimiza miaka miwili tangu afariki dunia, CCM imemlipa Shilingi Milioni 4.5 tu ikiwa ni sehemu ya malipo hayo huku akifuatilia kwa muda mrefu bila mafanikio kupata kiasi kilichobaki cha Shilingi milioni 70.5 bila mafanikio.

Komba aliyezaliwa mwaka 1954, alifariki dunia Februari 28, 2015 na kuzikwa Mkoani Ruvuma ambako enzi za uhai wake alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake katika kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali za kwaya, hasa za kukipigia debe chama chake (CCM) wakati wa kampeni mbalimbali za uchaguzi.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )