Saturday, March 25, 2017

Kauli ya Waziri Dkt Mwanyekembe kuhusu madai ya RC Makonda kuvamia Clouds

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, jana baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es salaam, amekiri kuwa anafahamu kuhusu tukio la uvamizi lililofanyika katika ofisi za Clouds Media Group.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Mwakyembe aliyechukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye alisema kuwa yeye kwa sasa hawezi kulizungumzia tukio hilo wala kutoa uamuzi wowote kwa kuwa hajapata ushahidi unaojitegemea.

“Ninachokijua kuhusu hilo tukio kinatokana na taarifa za vyombo vya habari, taarifa za magazeti, za redio, za televisheni, na sidhani kama taarifa hizo zinatosha kwa mimi kutoa uamuzi wowote.”

Ameongeza kuwa bado suala hilo ni la kuchunguzwa zaidi kwani picha inayotolewa ni ya upande mmoja.

“Mlalamikaji hapa ni Clouds, anayetupa taarifa kuhusu suala hili zima ni Clouds na wenzake. Kwa hivyo naipata picha hii kwa upande mmoja…”

Aidha kwa mujibu wa ripoti iliyokuwa imetolewa na kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri, Nape Nnauye ilisema kuwa wamesikiliza upande wa mlalamikaji (Clouds Media Group).

Lakini walipokwenda kwa ajili ya kuusikiliza upande wa mlalamikiwa (RC Paul Makonda) hawakufanikiwa kumpata. 

Hii ni baada ya wao kusubirishwa kwa muda mrefu  nje ya ofisi yake na baadae kuambiwa kuwa Makonda ameondoka na hatoweza kurudi kwa siku hiyo. Jambo hili liliwafanya wajumbe hao kujiaminisha kuwa Makonda hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo na aliamua kuwatoroka.

Hata hivyo ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Waziri, Nape Nnauye ili aifikishe katika mamlaka husika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )