Friday, March 3, 2017

Mgombea Ubunge CHADEMA auawa kikatili

Kada wa Chadema katika Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, Anitha Swai ameuawa katika tukio lililogubikwa na wingu zito.

Taarifa za awali zilizopatikana usiku wa kuamkia  leo zimedai kuwa Anitha ambaye aligombea ubunge wa viti maalum mwaka 2015, alitekwa nyara wilayani Rombo na kuuawa maeneo ya TPC nje kidogo ya mji wa Moshi.

Vyanzo mbalimbali vya habari vimedokeza kuwa mara ya mwisho mwanasiasa huyo alionekana akiwa na watu wawili wilayani Rombo siku ya Jumatatu, Februari 27 na kuaga wanaelekea Arusha.

Hata hivyo, tangu siku hiyo Anitha hakuonekana hadi maiti yake ilipogunduliwa jana (Alhamisi) jioni maeneo ya TPC huku gari lake likiwa limetelekezwa maeneo ya Bomambuzi mjini Moshi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kuokotwa kwa mwili huo, lakini amekataa kuthibitisha kama ni wa kada huyo wa Chadema.

"Ni kweli kuna tukio hilo, lakini ninachoweza kusema bado hajatambuliwa na mwili wake umepelekwa KCMC ili ndugu waweze kuutambua," amesema.

Hata hivyo, Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Mawenzi mjini Moshi, Hawa Mushi amethibitisha kuwa aliyeuawa ni kada wa chama chao, lakini chanzo na nani waliohusika hakijajulikana.

Hawa amesema taarifa zilizothibitishwa ni kuwa mwili wake ulipatikana maeneo ya TPC huku simu iliyopatikana katika gari yake ndiyo iliyosaidia kumtambua.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )