Saturday, May 6, 2017

VIDEO: CCM Yazungumzia Kutoonekana Hadharani kwa Katibu mkuu wa Chama Abdulrahman Kinana

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimempa mapumziko ya muda ambao hakijautaja Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.

Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, kiongozi huyo ameruhusiwa kupumzika ili kuangalia afya yake hadi hapo itakapoimarika.

Polepole alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake iliyolenga kukagua uhai wa CCM mkoani Arusha, ikiwa ni eneo linalotajwa kuwa ngome ya chama kikuu cha upinzani, Chadema.

Kauli hiyo ya Polepole imekuja ikiwa ni muda sasa Kinana hajaonekana hadharani, hatua ambayo imezusha maneno mengi, huku baadhi wakienda mbali na kuhusisha kitendo hicho na mgomo kutokana na uamuzi wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kumvua uwaziri wa Habari, Vijana Sanaa na Michezo ‘kijana wake’, Nape Nnauye.

Kuwapo kwa hisia za namna hiyo kunatokana na kile ambacho CCM ilidai kuwa ni uvumi, kwamba Kinana alitaka kuitisha mkutano na wanahabari siku moja baada ya Nape kuondolewa kwenye wadhifa huo na saa chache baadaye wakati akielekea kuzungumza na vyombo vya habari kutishiwa kwa bastola na mtu ambaye haijajulikana anafanya kazi wapi.

Ni wakati huo Rais Magufuli alilazimika kuzungumzia mahali alipo Kinana, akisema alikuwa amemtuma kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.

Rais Magufuli alitoa ufafanuzi huo wakati akiwaapisha Mawaziri Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Dk. Harrison Mwakyembe aliyechukua nafasi ya Nape.


 Hadi sasa hakuna picha yoyote inayomwonyesha kiongozi au mtu yeyote amefika nyumbani kwa Kinana kwa ajili ya kumjulia hali, jambo ambalo limezidi kuzua maswali.

 “Hili swali la Katibu wetu Mkuu ndugu Komrade Abdulrahmani Kinana limesemwa sana na mimi ninafurahi kwamba tunaanza kurejesha utamaduni ambao maisha ya viongozi wetu yanakuwa sehemu na maslahi ya umma wa Watanzania,” alisema Polepole na kuongeza:

“Lakini unapoona Katibu wetu Mkuu wa CCM anaulizwaulizwa yuko wapi na hata watu wasiokuwa wana CCM, hii inaonyesha kiwango cha imani cha Watanzania kinarejea kwa kasi kubwa, hasa katika kipindi hiki tunapofanya mageuzi makubwa ndani ya chama chetu.

“Na kwa hakika najua viongozi wa vyama vingine wasioonekana hawauliziwi na mtu yeyote, kwetu sisi ni dalili njema sana. Nipende tu kuwaambia jana nimeongea na Komrade Kinana bado yuko kwenye mapumziko ya kujitizama afya yake.

“Ninyi wote ni mashahidi mzee wetu huyu alifanya kazi kubwa ndani ya CCM na kwenye Serikali na pia kwenye wigo wa kimataifa, hasa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

“Lakini amefanya kazi kubwa zaidi kwenye chama ya kukijenga na kukiimarisha, hasa kwenye uongozi na utendaji kama Mtendaji Mkuu wa Chama.

“Leo labda niseme kwa sehemu mpaka wakati tunamaliza Mkutano Mkuu Maalumu ambao ulipitisha marekebisho na mabadiliko ya Katiba Ndugu Komrade Kinana alikuwa anafanya yote haya, lakini akiwa mgonjwa, akiugulia na sisi kwenye chama tuna utaratibu na tunawapenda viongozi wetu.

“Kwa hiyo ikakubalika achukue muda wa kutosha wa kuitazama afya yake nje ya nchi na kiongozi wa aina yake anaporejea, mgonjwa akitoka hospitali hakimbilii kazini au shambani moja kwa moja, inashauriwa kitaalamu atumie muda wa kupumzika ili kuimarisha afya yake.

“Na jana (juzi) nimezungumza naye anaendelea vizuri, yuko madhubuti kabisa kuliko jana, kwa hiyo nashukuru wale wote wanaofuatilia habari zetu za CCM na iwe mfano kwa vyama vingine,” alisema.   .

==>Msikilize hapo chini akiongea

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )