Saturday, May 13, 2017

Wanafunzi Watatu Walionusurika Katika Ajali Iliyoua 35 Kesho Watapelekwa Marekani Kwa Matibabu Zaidi

Watoto watatu walionusurika katika ajali basi iliyosababisha vifo vya wanafunzi, walimu pamoja na dereva wake mjini Arusha wanatarajiwa kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu zaidi nchini Charlotte North Carolina mwishoni mwa juma hili.

Mwinjilisti maarufu duniani kutoka Shirika la Samaritan Purse, Bill Graham wa Marekani ndiye aliyebeba gharama za kukodisha ndege maalumu aina ya DC 8 kupeleka wanafunzi waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani Karatu, Arusha.

Watoto hao wameumia shingo, miguu na sehemu mbalimbali za miili yao. 

Kwa mujibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyarandu aliyezungumza jana na waandishi wa habari mjini Arusha, gharama za kukodisha ndege kwenda Marekani si chini ya dola za Kimarekani 350,000 (Sh milioni 700). Gharama hizo ni nje ya matibabu, chakula na malazi kwa wakati wote ambao wagonjwa hao na wasindikizaji watakuwa nchini humo.

“Tumefanikiwa kupata ndege aina ya DC 8 kutoka Shirika la Samaritan Purse linaloongozwa na mtoto wa Billy Graham aitwaye Franklin kwa ajili ya kuwasafirisha watoto Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo na wazazi wao watatu, yaani mama zao,” alisema Nyalandu akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Alisema pia watoto hao wataambatana na daktari wa hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Elias Mashalla na muuguzi Simphorosa Silalye. 

Kwa mujibu wa Nyalandu, ndege hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA) leo jioni ikitokea Charlotte ,Jimbo la North Carolina, Marekani.

“Endapo taratibu za safari ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa visa utafanikiwa, basi ndege inaondoka na wagfonjwa na wasindikizaji Jumapili (kesho) na baada ya kufika mjini Charlotte, North Carolina watasafiri kwa ndege nyingine maalumu ya kubeba wagonjwa hadi mji wa Sioux City, Iowa ambako watapokelewa na uongozi wa Hospitali ya Mercu na Shirika la STEMM,” alisema Nyalandu.

Alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kupongeza juhudi za Rais, Dk John Magufuli, Makamu wake, Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Mkoa wa Arusha chini ya Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo kwa kuguswa na kushiriki katika kila hatua kuanzia baada ya ajali, mazishi hadi ufuatiliaji wa afya za majeruhi.

‘’Hili jambo ni letu sote hapa, hatuhitaji sifa bali tunachopaswa Watanzania wote kushirikiana kwa pamoja na kuweka mbele ubinadamu na kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia hawa watoto ili waweze kupata nafuu na kurudi shuleni,” alisema 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo alisema kuwa katika michango yote iliyochangwa kwa ajili ya rambirambi kwa msiba huo mpaka jana zilipatikana fedha kiasi cha Sh milioni 215.

Gambo alisema katika fedha hizo, kila familia ilikabidhiwa zaidi ya Sh milioni 3.8 na pia Serikali ilibeba gharama za usafiri, majeneza, mafuta ya magari na malipo ya madereva. 

Alisema Sh milioni 190 zilitumika katika matumizi mbalimbali ya msiba huo na kuwataka walioahidi kuchangia kutimiza ahadi zao.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )