Tuesday, July 18, 2017

CHADEMA Yalia na Wahisani......Yataka Waungane Kuinyima Tanzania Misaada

Siku moja baada ya kuachiwa kwa dhamana viongozi wake, Chadema imetaka jumuiya ya kimataifa kuacha kuifadhili Tanzania, ikidai kuna ukiukwaji wa demokrasia na haki za binadamu.

Tamko hilo lilitolewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alipozungumza na waandishi wa habari jana kuhusu kuendelea kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho, akiwemo Dk Vicent Mashinji, ambaye ni katibu mkuu aliyekamatwa Jumamosi akiwa Mbambabay wilayani Nyasa.

Wengine waliokamatwa ni Cecil Mwambe, ambaye ni mwenyekiti wa Kanda ya Kusini na mbunge wa Ndanda, Philbert Ngatunga (katibu wa kanda) na Manawa Samuda (ofisa wa operesheni na mafunzo).

Pamoja nao ni Zubeda Sakuru (mbunge wa viti maalum, Ruvuma), Asia Mohamed (ofisa wa kanda), Ireneus Ngwatura (mwenyekiti wa Mkoa wa Ruvuma), Delphin Ngaiza (katibu wa Mkoa wa Ruvuma), Cuthbert Ngwata (mwenyekiti wa Wilaya ya Nyasa) na Charles Makunguru (katibu wa uenezi wa Wilaya ya Nyasa).

Ilikuwa ni siku chache baada ya viongozi na wanachama 51 kukamatwa Julai 8 wakiwa kwenye kikao cha ndani wilayani Chato mkoani Geita.

Vitendo hivyo viliifanya Chadema itoe tamko zito jana.

“Nchi zinazoupa fedha uongozi wa Rais (John) Magufuli, hazina budi kuacha,” alisema Lissu akitoa mfano wa jinsi Afrika Kusini ilivyotengwa wakati wa siasa za ubaguzi.

“Hawatakiwi kupewa fedha ambazo zitakandamiza Watanzania, ambazo zitauza demokrasia.”

Lissu, ambaye anajulikana kwa kutumia maneno mazito, alito mifano mingi aliyodai inaonyesha kukandamizwa kwa demokrasia.

“Wao wanafanya mikutano ambayo sisi tumezuiwa, wanafanya mikutano ya ndani ambayo sisi tumezuiwa,” alisema Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki.

Lissu alisema sasa ni wakati wa kuacha woga na badala yake kupaza sauti kimataifa kupinga, kile alichoita ni ukandamizaji wa demokrasia ili wahisani wainyime misaada Serikali ya Tanzania.

Mwanasheria huyo alihoji kitendo cha majaji wa Mahakama Kuu kujiuzulu bila kujulikana sababu licha ya baadhi yao kuhusishwa na sakata la uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT).

Lissu pia alizungumzia matumizi ya Jeshi la Polisi akishauri lisiendelee kutumika kukamata wanasiasa wa upinzani ambao wanafanya mikutano na vikao vya ndani kwa kuzingatia sheria na Katiba, badala yake litumike kukamata wahalifu.

“Kila Polisi aliyenikamata anasema ‘bwana we tumeagizwa kutoka juu’. Sasa hili ni jeshi la maagizo au ni Jeshi la Polisi?” alihoji Lissu, ambaye amewahi kukamatwa mara kadhaa na kulala mahabusu.

Mwanasheria huyo wa kujitegemea alisema kupinga Serikali si dhambi na haijawahi kuwa dhambi wala kosa la jinai. Pia, alisema kama unatoa kauli kwa kuonyesha ubovu au kukosoa, si uchochezi.

Akijua kuwa alikuwa akitoa kauli kali dhidi ya Serikali, Lissu alisema anaamini waandishi wa habari hawataandika yote aliyosema kwa sababu wanaogopa sheria zilizopo, maonyo na vitisho.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )