Sunday, July 2, 2017

Rais Magufuli: Tanzania ni Yetu, Selous Iko Tanzania......Tuna Uhuru wa Kuamua Mambo Yetu maana Tumechoka Kuchezewa

Rais  John Magufuli amesema ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) mkoani Pwani lazima ufanyike, akiapa kuwa inyeshe mvua au liwake jua, lazima utajengwa.

Alisema hayo jana alipokuwa akifungua Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), barabara ya Kilwa.

Aliwaeleza wawekezaji kuwa changamoto ya umeme wa uhakika itakwisha, kwani Tanzania itakuwa na umeme wa megawati kati ya 4,000 na 5, 000 utakapokamilika mradi huo.

“Inyeshe mvua, liwake jua Stiegler’s Gorge itajengwa, tumeamua kuchukua juhudi za makusudi kuifufua na ninawahakikishia wawekezaji tunaifufua... na tunaanza kwa fedha yetu,” alisema Rais Magufuli.

Aliwahakikishia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwa Tanzania imejipanga vizuri, kuweka mazingira mazuri kutatua changamoto za sekta ya viwanda. 

“Moja ya changamoto kubwa ni suala la umeme, kama serikali tumeamua kuchukua jitihada za makusudi kutekeleza ahadi za Mwalimu Nyerere ya kuendeleza Stiegler’s Gorge kwa kujenga bwawa kubwa,” alisema.

Alisema ameshatoa maelekezo kwa wizara husika, pia imeundwa timu ya wataalamu wa kufuatilia na kwamba zabuni itakapotangazwa, watu wajitokeze kwa ajili ya ujenzi. 

Alisema ujenzi wa bwawa hilo, utawezesha kupatikana umeme wa megawati 2,100, ikimaanisha kuwa ni umeme utakaotosheleza mahitaji mengi, yakiwemo ya matumizi ya kawaida, viwandani na mengineyo.

“Najua wapo watakaojiuliza fedha kweli wanazo? Nataka kuwaambia fedha tunazo, haiingii akilini tunazungumzia viwanda wakati umeme hatuna,” alisema. 

Aliongeza kuwa, Serikali ikiomba fedha za mradi huo kwa wafadhili, wataweka masharti makubwa na kuambiwa mradi huo una matatizo ya kimazingira.

“Nataka kuwaambia kuwa hatutasikiliza suala la environmental impact (athari za kimazingira), Selous iko Tanzania, tunawajibu wa kuamua jambo la kufanya ambapo,” alisema Rais na kuongeza kuwa mradi huo, utatumia asilimia tatu tu ya hifadhi hiyo.

Alisema kwa watu ambao wanazingatia mambo ya kimazingira, wataona kwamba Tanzania inatunza mazingira, kwani yatapatikana maji kwa ajili pia ya uvuvi, viumbehai wengine watatumia pia maji hayo kwa kilimo.

Rais Magufuli aliwaomba wadau wa maendeleo ambao wana nia ya kuisaidia Tanzania, wajitokeze ili Watanzania wanufaike na maliasili zao. 

Alisema umeme unaopatikana sasa hapa nchini ni megawati 1,460, lakini jitihada mbalimbali zimefanyika katika kuongeza kiwango hicho, ambapo ni pamoja na kuongeza umeme katika miradi ya Kinyerezi I, II na III iliyopo Dar es Salaam, itakayoongeza upatikanaji wa umeme nchini.

Rais Magufuli waliwaomba pia mabalozi wa nchi zote zenye uwakilishi hapa nchini, kuisaidia Tanzania kupitia nchi zao katika miradi mikubwa ambayo ina tija kwa taifa zima.

 “Kwa sababu tukishaweza kuzalisha megawati 2,100 watu wengi watakuwa na umeme, nina uhakika Waziri wa Mambo ya Nje atakuwa amechukua hiyo, na pia nawaomba mabalozi wote tunahitaji msaada katika miradi mikubwa,” alisema.

Rais Magufuli alipongeza maandalizi ya maonesho hayo, ambapo baada ya kuhutubia alipita kuangalia baadhi ya mabanda na kupata maelezo mbalimbali. 

Alisema maonesho hayo yana faida kubwa kwa wafanyabiashara, kwani huwakutanisha na wateja wao na pia kukutana na kampuni nyingine za nje na ndani ya nchi, kujifunza mambo mbalimbali na pia kubadilishana uzoefu na kuanzisha uhusiano wa kibiashara.

Alizipongeza pia kampuni za ndani na zile za nje takribani 3,000, zinazoshiriki katika maonesho hayo, zikiwemo 515 kutoka katika nchi 30 duniani. Rais Magufuli alisema Tanzania ni salama na ya amani na kwamba ipo kwa ajili ya wawekezaji.

Aliwataka Watanzania kutumia maonesho hayo, kama chachu ya kuibadili Tanzania. 

“Tumechoka, tumechezewa sana, lakini tulichezewa kwa sababu tuliamua sisi kuchezewa lazima tubadilike na moyo wa kubadili Tanzania tuanze sasa,” alisema Rais Magufuli.
Advertisement
tang
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )