Wednesday, July 26, 2017

Serikali Yawajibu ACACIA......Yasema TRA Iko Sahihi Kudai Kodi ya Trilioni 424 na Kama Hawaridhiki Wakate Rufaa

Siku Chache baada ya Kampuni ya Acacia kuonyesha kushitushwa na deni lililoelekezwa kwenye kampuni tanzu zinazodaiwa kodi ya dola za Marekani 190 (Sh trilioni 424) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), serikali imesema kama hairidhiki iende kwenye bodi ya rufaa ya kodi.

Kampuni hizo ni  Bulyanhulu Gold mine (BGML) inayoendesha mgodi wa Bulyanhulu na Pangea Minerals (PML) inayosimamia mgodi wa Buzwagi,.

Serikali pia imeelezwa kushangazwa na jinsi Acacia ilivyojiingiza kwenye suala hilo ikizingatiwa TRA ilipeleka madai ya kodi hizo kwa  BGML na PML.

Wakati hayo yakiendelea, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),   limeripoti kuwa  baada ya Acacia   kutoa taarifa juu ya madai ya kodi iliyoainishwa   na TRA, jana asubuhi kwenye soko la hisa la London, hisa za kampuni hiyo ziliporomoka kwa asilimia 7.7.

Taarifa ya TRA kuzidai kampuni hizo matrilioni ya shilingi  imetolewa  ikiwa ni miezi michache baada ya Kamati ya Rais iliyoongozwa na Profesa  Nehemiah Osoro, kutoa taarifa yake   kuonyesha Acacia imekuwa ikiibia serikali  fedha nyingi kwenye mchanga wa dhahabu (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi.

Ilionyesha pia kuwa Acacia inaendesha shughuli zake nchini kinyume cha taratibu kwa sababu haijasajiliwa.

Baada ya taarifa hiyo kutolewa, Juni 14, Rais Magufuli alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation Profesa John Thornton,    Dar es Salaam.

Baadaye Ikulu  ilitoa taarifa kuwa Barrick inayomiliki zaidi ya asilimia 60 ya migodi hiyo, ilisema  ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Wizara ya Fedha na Mipango, Beny Mwaipaja, jana  alisema deni hilo ni halali na lilikokotolewa kwa mujibu wa sheria  na endapo wadaiwa wana tatizo, wanajua sehemu ya kwenda.

“TRA iliwasilisha deni hilo kwa kampuni za Bulyanhulu na Pangea na wala siyo Acacia, kama wanaona wameonewa, wawasilishe malalamiko yao kwa Kamishna wa TRA au bodi ya rufani za kodi, yatafanyiwa kazi,”alisema Mwaipaja.

Alisema kampuni za uwekezaji zinajua utaratibu wa kufuata kama zinaona kuna tatizo, hivyo basi Acacia ina muda wa kutosha wa kuwasilisha malalamiko yake kwenye mamlaka zinazohusika kuliko kulalamika bila ya kufuata utaratibu.

“Kila mgodi umepelekewa bili yake kasoro Acacia ambao bado hawajapelekewa bili,”alisema.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema   masuala yanayohusu mlipakodi, kwa mujibu wa sheria Mamlaka  hairuhusiwi kuyajadili hadharani bali huwasiliana na mhusika moja kwa moja.

“Issue (suala) za mlipakodi kisheria haturuhusiwi kuzi-discuss in public (kuzijadili hadharani) huwa tunawasiliana na mlipakodi moja kwa moja,”alisema Kayombo.

Taarifa ya ACACIA
Taarifa ya Acacia juzi ilisema TRA  inaonyesha kuwa migodi yake ya Bulyanhulu inadaiwa kodi ya kati ya mwaka 2000 hadi 2017  wakati Pangea inadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.

Taarifa yake inasema uchambuzi uliofanywa na TRA umeonyesha Mgodi wa Bulyanhulu unadaiwa dola za Marekani bilioni 154 (Sh trilioni 344.8) na Mgodi wa Pangea dola bilioni 36 (Sh trilioni 76.1).

Inasema dola bilioni 40 (Sh trilioni 89.5 trilioni) ni malimbikizo ya kodi na dola bilioni 15 (Sh trilioni 335.9) ni adhabu na riba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti ya kampuni hiyo, kodi hiyo imetokana na ripoti za kamati mbili za Rais zilizoonyesha kuwa kampuni hizo zimekuwa hazitangazi kiasi halisi cha mapato yake yanayotokana na makinikia.

Hata hivyo, Acacia ilisema inaendelea na msimamo wake wa kupinga matokeo ya kamati hizo ikisisitiza imekuwa ikitangaza mapato yake yote.

Kampuni hiyo ilisema bado haijapata nakala za ripoti za kamati ya kwanza na ya pili zilizowasilishwa kwa Rais Magufuli Mei 24 na Juni 12 mwaka huu.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )