Monday, July 3, 2017

Uchaguzi mkuu TFF wasimamishwa

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) imesimamisha shughuli zote za uchaguzi kuanzia jana Jumapili hadi Julai 4 ambapo watakaa kikao cha kamati hiyo na kutoa maamuzi yatakayofikiwa kuhusu mchakato huo.

Sababu kubwa imeelezwa kuwa ni wajumbe wa kamati ya uchaguzi ya TFF kukataa majina ya baadhi ya wagombea kwa sababu binafsi. 

Revocatus Kuuli ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi amesema kutokuwa na maelewano kumemsababisha achukue uamuzi wa kuuandikia barua Kamati ya Utendaji akiiomba isitishe mchakato wa uchaguzi (kwakuwa kanuni zilizopo zinamruhusu kufanya hivyo) japo kumekuwa na taarifa kuwa Bwana Kuuli alitofautiana na wajumbe wengine wa Kamati ya Uchaguzi kuhusu hatma ya Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi ambaye alichukua fomu kutaka kutetea kiti chake.

Mgogoro uliosababisha kutoelewana huku umetokana na wajumbe wanne kati ya watano kutaka jina la Rais wa sasa, Jamal Malinzi, lipitishwe bila kuwapo – jambo ambalo Revocatus Kuuli anasema si sahihi kikanuni.

 Kamati ya Uchaguzi ya TFF ina wajumbe watano. Kwa sababu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Mkuu wa TFF Revocatus Kuuli akaiandikia barua Kamati ya Utendaji ya TFF akitaka mchakato mzima wa uchaguzi usimamishwe na kuangalia kama Sheria za zoezi zima zinazingatiwa.

“Kikao chetu cha leo kimefanyika lakini hakijatoa maamuzi ya matatizo yaliyotokea jana.”

“Mimi kama Mwenyekiti wa Kamati nimechukua maamuzi ya dhamana niliyonayo. Nimemuandikia Katibu juu ya dhamira yangu kuangalia upya mwenendo mzima wa kamati. Wamekubaliana na maombi yangu na wamenipa barua kwamba wanaona sahihi mchakato mzima usimame mpaka matatizo yaliyotokea yatakapopelekwa kwenye Kamati ya Utendaji ambayo ndio yenye mamlaka ya mwisho.”

“Wamesema wataitisha kikao Julai 4, 2017 (Jumanne ijayo). Matatizo yalikuwa mengi, kuna watu wamekatakata majina kwa uonevu tu. Taratibu zinataka kupindishwa kwa sababu ya kutaka kupendelea watu fulani.”

“Mimi siwezi kuwa sehemu ya kamati ambayo ipo namna hii, kwa hiyo nashukuru barua yangu imepokelewa na imefanyiwa kazi kama nilivyokuwa nimetaraji.”

Julai 4, 2017 baada ya Kamati ya Utendaji kukaa na kujadili mgogoro huo uamuzi wa kuendelea au kutoendelea kwa mchakato wa uchaguzi huo utatolewa.

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Salum Madadi amesema amekubali ombi la Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kuhusu kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF kutokana na kutofautiana kwa wajumbe wa kamati hiyo.

Madadi amesema Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana Jumanne Julai 4, 2017 kwa ajili ya kulitolea uamuzi suala hilo.

“Kumetokea mgawanyiko ndani ya kamati yetu ya uchaguzi, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ametuandikia barua na tumeshauriana naye kusitisha mchakato wa uchaguzi na tumeitisha kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ya TFF tarehe 4 Julai, 2017 saa 7:00 mchana.”

“Baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji tutakuwa na cha kusema kuhusu mchakato wa uchaguzi,” alisema Madadi.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )