Sunday, July 2, 2017

Watanzania 18 watekwa na waasi wa Congo

Waasi wanaodaiwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamewateka madereva 21, wakiwamo Watanzania 18 wanaofanya kazi kwenye kampuni ya malori ya mizigo ya Alistair ya nchini.

Meneja usimamizi wa Tanzania na DRC wa kampuni ya Alistair , Anna Joyce Mbise aliliambia gazaeti la Mwananchi  jana kuwa  madereva hao walitekwa asubuhi ya Juni 29, baada ya mapambano kati ya askari wa Serikali ya Congo na waasi hao.

“Kwa mujibu wa maelezo ya madereva hao ni kwamba askari wa Serikali waliokuwa wanawasindikiza kabla ya msafara kuvamiwa, walizidiwa kwenye mashambulizi hayo ndipo wakatekwa,” alisema Mbise na kuongeza:

“Wametueleza kuwa hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo, waasi wamekuwa wakizungumza nao vyema, lakini gari zetu tatu zimeharibika kwa risasi kutokana na mashambulizi hayo,” alisema.

Alisema kampuni hiyo imewasiliana na viongozi husika wa Serikali kwa kuandika barua Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ili wasaidie madereva hao kuachiwa huru wakiwa salama.

“Tumejawa na hofu kuhusu usalama wao, kwani tunaamini kwamba askari wa jeshi la Serikali lazima wanajipanga kurejea kupambana ili kulikomboa eneo hilo, hapo tuna wasiwasi na usalama wa madereva hao ,” alisema.

Mratibu wa Shirikisho la Wasafirishaji Afrika Mashariki (FEARTA), Emmanuel Kakuyu alisema taarifa walizonazo ni kwamba madereva hao wamekumbwa na mkasa huo katika eneo la kijiji cha Lulimba kilichopo kati ya Ziwa Tanganyika na Kindu Manyema.

Alisema waasi hawa hawajawadhuru madereva hao, lakini alifafanua kuwa madereva watatu kati ya 21 wanatoka Uganda.

“Watekaji wamekuwa wakizungumza nao vizuri ikiwamo kuwahakikishia usalama wao wakidai kwamba hawana ugomvi nao, bali wana ugomvi na Serikali ya Congo,” alisema.

Umbali kati ya Lulimba na Kigoma ni kilomita 448, lakini ili ufike Lulimba ni lazima ulizunguke Ziwa Tanganyika upande wa mashariki mwa DRC.

Kaimu Mkurugenzi wa dawati la Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Suleiman Saleh alijibu kwa kifupi kwamba wamepokea taarifa za utekaji huo na tayari wameanza kushughulikia.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )