Sunday, July 30, 2017

Waziri Mkuu Azindua Meli mbili zilizonunuliwa na Serikali Mkoani Mbeya

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amezindua Meli mbili za mizigo za Mv Njombe na Mv Ruvuma zitakazotumika katika kusafirishia mizigo kwenye Ziwa Nyasa na kuonya kwamba zisitumike kama eneo la kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya.

Amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Meli hizo zilizogharimu sh. bilioni 11.253 ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli alizozitoa ikiwa na lengo la kutatua changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo katika Ziwa Nyasa.

Amesema kuwa ni jambo la faraja na la kujivunia kwa Serikali na wananchi kwa pamoja kushuhudia meli zilizotengenezwa na Mtanzania, zikiwa zimekamilika tayari kwa kuanza kazi ya kuwahudumia wananchi, ambapo awali suala hilo lilikuwa likifanywa na raia wa kigeni.

Waziri Mkuu amezindua meli hizo zilizojengwa na kampuni ya Kitanzania ya M/S Songoro  Marine Transport  jana katika bandari ya Kiwira wilayani Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.

Aidha, alisema kuwa Meli hizo zitumike katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kusafirisha mizigo na biashara halali kati ya nchi za Tanzania na Malawi na zisitumike kama eneo la kuingiza wahamiaji haramu pamoja na dawa za kulevya nchini.

“Changamoto ya usafiri wa mizigo katika ziwa Nyasa itakuwa historia kwani meli hizi zitarahisisha usafiri na kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania nan chi za Malawi na Msumbiji, hivyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kutoa ahadi hii ambayo leo utekelezaji wake umekamilika.”

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Karim Mataka alisema kuwa ujenzi wa meli hizo ulianza Juni 2015 na zina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo kwa kila moja.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )