Monday, August 28, 2017

ACT Wazalendo kudai mikutano ya hadhara mahakamani

Chama cha ACT-Wazalendo kimepanga kufungua shauri Mahakama Kuu kupinga amri ya kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa wale ambao hawakushinda kwenye uchaguzi katika majimbo husika.

Chama hicho kimefikia uamuzi huo kupitia Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia wa pili uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Taarifa ya mkutano huo iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa chama hicho kimeamua kufungua shauri hilo kudai haki ya kufanya mikutano ya hadhara ambayo ni shughuli halali za vyama vyote vya siasa kwa mujibu wa katiba.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa mbali na kufungua shauri hilo, wameazimia kumuandikia barua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumuomba atengue zuio la kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

“Maazimio haya yote yatapelekwa kwenye idara husika za chama kwa ajili ya kutekeleza mara moja. Pia, viongozi wa chama wataendelea kuipigania misingi ya kidemokrasia,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

ACT Wazalendo walishinda jimbo moja pekee la ubunge la Kigoma Mjini ambapo kwa mujibu wa masharti ya kufanya mikutano ya hadhara ndilo jimbo pekee ambalo chama hicho kinaweza kufanya mkutano wa hadhara wa jimbo.

Zitto Kabwe ambaye ni Kiongozi Mkuu wa chama hicho ndiye mbunge pekee anayekiwakilisha bungeni.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )