Friday, September 22, 2017

Mbowe Aipinga Serikali Sakata la Kumsafirisha Tundu Lissu

Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA Mh. Freeman Mbowe, amesema Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu hatosafirishwa kwenda popote mpaka pale madaktari watakaporuhusu.

Mhe. Mbowe ameeleza hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari ikiwa imepita siku moja tokea serikali ya Tanzania itoe kauli yake kuwa ipo tayari kumtibia Lissu popote pale duniani kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu.

"Tundu Lissu bado ni mgonjwa sana, hawezi kusafirishwa nje ama kutikiswa kwa njia yeyote katika kipindi hiki kwa hiyo mpango wowote wa kumuondoa hospitalini Nairobi kumpeleka nchi yeyote hautokuwepo kwa sasa mpaka hapo madaktari watakaporuhusu kulingana na hali yake", amesema Mbowe.

Pamoja na hayo, Mbowe ameendelea kwa kusema "Madaktari wametuhakikishia wana vifaa, dawa, utaalamu wa kukamilisha awamu ya pili ya matibabu ya Mhe. Lissu na yatafanyika hapo hapo katika hospitali ya Nairobi, Kama kutakuwa na ulazima katika hatua za baadae basi hizo zitafanyika kulingana na ushauri wa madaktari".

Aidha, Mbowe amesema wamelazimika kumuwekea ulinzi mkubwa Lissu katika hospitali aliyolazwa kutokana na kuhofia hali ya usalama iliyokuwa imetanda juu ya Mbunge huyo kutokana na shambulio alilofanyiwa na watu waliokosa utu.

"Nipende kusema tunawashukuru sana uongozi wa hospitali ya Nairobi, wenzetu walielewa hofu yetu na wametoa ulinzi wa ziada kwa ajili ya Mhe. Lissu masaa 24 ndani na nje. Kwa hiyo Lissu yupo chini ya uangalizi mkali sana na hili lilifanyika kutokana hofu iliyotanda na inayotanda kwa halali kabisa kwa sababu kuna watu walitaka kuondoa maisha ya Lissu lakini hawakuweza kufanikisha kazi yao, na hao watu hawana utu kabisa kwani tukiwapa nafasi hawatasita kukamilisha kazi yao", amesisitiza Mbowe.

Kwa upande mwingine, Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na watanzania kwa ujumla kutokuwa na hofu kuhusu Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kwani madaktari wameshawahakikishia kuwa Lissu atapona na kurudi kuendelea katika harakati zake alizokuwa anazifanya kama awali.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )