Thursday, September 7, 2017

Msimamo wa CUF ya Maalim Seif baada ya Wabunge wa Lipumba kuapishwa

Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Maalim Seif kimetangaza misimamo yake baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwaapisha wabunge viti maalumu saba walioteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi linalomuunga mkono Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati akitangaza misimamo ya CUF mbele ya Wanahabari, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Mbarala Maharagande amesema Baraza Kuu la Uongozi la Taifa CUF haliwatambui wabunge hao walioapishwa Septemba 5.

Mbarala amesema CUF haitokubali kutumiwa kutengeneza upinzani bandia wa kisiasa wa kuendelea kuisaidia CCM kubaki madarakani, na kudai kwamba haiko tayari kushirikiana na wabunge hao kwa kuwa wameteuliwa kwa ajili ya kuisaidia CCM Bungeni.

“Jana tumeshuhudia jinsi wafuasi wa Lipumba walivyopokelewa na wabunge wa CCM Dodoma na kuandaliwa dhifa ya kusherehekea ushindi wa hujuma dhidi ya CUF. Hii ni mara ya kwanza kaa wanaoitwa wabunge wa Upinzani kuingia bungeni kuapishwa na kusindikizwa na wabunge wa CCM,” amesema.

“Kwa hakika spika amepoteza sifa na haiba ya kuongoza Bunge ambalo ni mhimili wa dola na ambao ulipaswa kuwa alama ya uadilifu katika nchi, lilipaswa kuwa chombo muhimu cha watanzania katika kuisimamia serikali ili wananchi wapate maendeleo, lilipaswa kuwa huru chenye kujisimamia na kuacha kutumiwa kukandamiza upinzani. Ajitathimini aone kwamba anahitaji watanzania wamkumbuke kwa jambo lipi baada ya kuondoka katika nafasi hiyo,” amesema.

Wakizungumza katika mkutano huo baadhi ya wabunge waliovuliwa ubunge wao, wamezitaka baadhi ya taasisi za serikali kutoshiriki katika kuhujumu mfumo wa demokrasia.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Riziki Ngwali amesema anasikitishwa na kitendo cha Bunge kuwaapisha wabunge hao kwa madai kwamba kimelenga kuugandamiza mfumo wa demokrasia.

“Inasikitisha, nchi ambayo ni ya kidemokrasia imeweka sheria na taratibu za kusimamia mifumo ya demokrasia, halafu taasisi zinashiriki kuuharibu mfumo huo. Sikutegemea kama ofisi ya msajili ingefanya hivyo, ni muendelezo wa njama na hujuma,” amesema na kuongeza.

“Nilimtahadharisha msajili kwamba anachokifanya kinahatarisha usalama, CUF ni chama chenye nguvu hasa upande wa Zanzibar. Hivi vilio vya kila mara haviwezi vikaisha kimya kimya. Kuna mwisho na kikomo, hujuma haisaidii, mkinya haki watu wataitafuta.”

Kwa upande wake Savelina Mwijage amesema

“Sisi hatulilii kuvuliwa kwetu ubunge, tunalilia kuathirika kwa chama chetu. Sisi ni wanadamu hatuwezi kusema lolote Mungu ataamua na mahakama pia itaamua, Spika anachuki na CUF si vingine,” amesema.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )