Wednesday, September 6, 2017

Raila Odinga kugoma kushiriki uchaguzi wa marudio Kenya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raia Odinga amesema kuwa hatoshiriki katika uchaguzi mkuu wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 7 mwaka huu kama michakato muhimu ya kikatiba na kisheria haitawekwa sawa.

Raila Odinga alisema mbali na michakato hiyo ambayo hakuiweka bayana alisema pia lazima mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) yafanyike ili kuondolewa kwa maafisa ambao walisababisha kuharibika kwa uchaguzi mkuu uliopita.

“Tunajua ambacho tume ya uchaguzi ilifanya, ndio sababu tunasema kuwe na mabadiliko kwani tukirudia uchaguzi na watu hao hao matokeo yatakuwa yale yale,”  alisema Odinga.

Mapema juma lililopita Mahakama ya Juu nchini Kenya ilitangaza kuwa uchaguzi mkuu wa Agosti 8 ni batili kutokana na kukumbwa na kasoro nyingi.

Katika uchaguzi uliopita, Rais Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata 54%  huku akifuatiwa na Odinga aliyepata 45%.

Akizungumza na waandishi wa habari Odinga alisema kuwa, uchaguzi wa marudio unatakiwa kufanyika katika mazingira ambayo kila kilichokosewa katika uchaguzi uliopita kitaweza kurekebishwa.

Jumatatu Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Kenya ilitangaza kwamba uchaguzi mpya wa urais nchini humo utafanyika tarehe 17 Oktoba, 2017.

Mwenyekiti wa tume, Wafula Chebukati alisema uchaguzi huo utashirikisha wagombea wawili pekee wa urais, Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

Advertisement
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )