Wednesday, September 20, 2017

Rais Magufuli aagiza ukuta mkubwa kujengwa migodi ya Tanzanite

Rais John Magufuli ameagiza kujengwa uzio katika eneo linalozunguka machimbo ya Tanzanite liliko Simanjiro ikiwa ni hatua yake ya kutaka kukabiliana na utoroshwaji wa rasilimali hiyo.

Amelisisitiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanza kazi hiyo haraka iwezekanavyo.

Rais Magufuli ambaye yuko ziarani mkoani Manyara amesema vikosi vya ulinzi na usalama vinapaswa kushirikiana kujenga ukuta huo ambao utaanzia eneo la block A hadi D la machimbo hayo.

Baada ya ujenzi huo kukamilika ametaka kufungwa mitambo maalumu ikiwamo kamera zitakazokuwa na uwezo kutambua na kubaini matukio yoyote yanayotendeka katika eneo hilo.

“Nataka ukuta huu uanze mara moja tena JWTZ kupitia Suma JKT waanze kazi hii mara moja na baada ya kukamilika eneo hili liwe na mlango mmoja tu ambao utaweka mtambo wa ukaguzi... wewe ukiweka Tanzanite tumboni tutakubaini, ukiweka kwenye kiatu uonekane pia,” amesema Rais Magufuli.

Amesema lengo la Serikali kufanya hivyo ni kuhakikisha inapata sehemu ya mapato yake na wawekezaji waondoke na haki yao bila kupunjwa upande wowote.

Amesema hataki kuona rasilimali za Taifa zinatoroshwa kienyeji na kwenda kuwafaidisha wajanja wachache walioko nje ya nchi hivyo ili kudhibiti hali hiyo ameamua kuchukua hatua madhubuti.

“Hapa adui yetu siyo CCM au Chadema ama mwingine yeyote, adui yetu ni yule anayopora mali zetu, hatupaswi kugombana sisi wenyewe na kumuacha adui yetu yuko pembeni, naomba tushikamane katika hili maana hii vita ya uchumi siyo lelemama lazima tuwe wamoja,” amesema.

Pia, amesema ndoto yake ni kuona soko la Tanzanite linakuwa Simanjiro ili wafanyabiashara kutoka ng’ambo kama Marekani, India na Ulaya wanafika kwenye eneo hilo kufanya biashara.

“Tunataka soko la Tanzanite linakuwa hapa Simanjiro ili hawa wafanyabiashara wafunge safari waje kununulia hapa na hiyo itakuwa na manufaa pia kwa wafanyabiashara wa eneo hilo maana hata yule mchinja mbuzi ama mwenye gesti atafaidika na ujio huo,” amesema.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumatano wakati akizindua barabara ya kiwango cha lami ya Mererani yenye urefu wa kilometa 26 ambayo imegharimu kiasi cha Sh 32.5 bilioni.  Rais ameahidi kuendelea na kipande kilichobakia ili lami hiyo ifike makao makuu ya Mkoa wa Manyara ambayo ni Babati.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )