Friday, September 22, 2017

Tamko la Serikali Kuhusu Matibabu ya Tundu Lissu

Baada ya kushutumiwa kwamba imekaa kimya katika suala la matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Serikali imejitokeza na kueleza kwamba iko tayari kugharamia tiba yake popote pale ikiwa itaombwa na familia au kwa ushauri wa madaktari.

Lakini wakati Serikali ikisema hayo Lazaro Nyalandu ambaye amekuwa akifanya mipango ili Lissu apelekwe kutibiwa ng’ambo, amesema madaktari wa Nairobi alikolazwa wamesema hawezi kusafirishwa katika kipindi hiki.

Jana akiwa Tanga, Waziri wa Afya, Ummy Mwaimu aliitisha mkutano na wanahabari na kusisitiza kuwa Serikali haijashindwa kuchangia gharama za matibabu ya Lissu huku akisema tangu mwanzo wa tukio la kushambuliwa kwake kwa risasi Septemba 7 huko Dodoma, viongozi wamekuwa wakishirikiana na familia katika kunusuru maisha yake.

Alisema amesikitishwa na namna ya suala la matibabu ya Rais huyo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), linavyochukuliwa kisiasa huku akitahadharisha kwamba michango inayoendelea kuhamasishwa kusaidia kumtibu inaweza kutumiwa na matapeli kuwaibia wanaochanga.

“Serikali ina mpango wake katika kushughulikia matukio kama hayo, njia hiyo ndiyo iliyofanyika awali baada ya mbunge huyo kushambuliwa. Alifikishwa hospitalini na baadaye kukawepo na mpango wa kumpeleka Muhimbili,” alisema Ummy.

Baada ya shambulio hilo, Lissu alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya kusafirishwa kwa ndege ya kukodi hadi Nairobi, Kenya anakoendelea na matibabu.

Kabla ya kupelekwa Nairobi, Serikali kupitia Bunge ilieleza kwamba kwa utaratibu wake, mgonjwa anapopata rufaa hupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na ikishindikana anahamishiwa Apollo, India na si kinyume cha hapo.

 Utaratibu huo ulipingwa na viongozi wa Chadema ambao wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe waliamua kumpeleka Nairobi kwa walichoeleza kuwa ni kwa usalama wa mgonjwa.

Tangu alipopelekwa huko, Chadema imekuwa ikisema kwamba Serikali haijachangia chochote katika matibabu hayo ambayo tayari kiasi cha Sh160 milioni kimeshatumika ambazo zimetoka katika chama hicho na michango ya wananchi.

Lakini jana, Waziri Ummy alisema Serikali inasubiri familia iseme nini inataka kifanyike na wapi inataka mgonjwa wao akatibiwe na kwamba itakuwa nayo bega kwa bega kuhakikisha anatibiwa popote duniani na kwa gharama yoyote ile na si kwa michango ya wasamaria wema.

Alisema lengo la Serikali ni kuondoa dhana kwamba imejitenga katika matibabu ya Lissu hadi jukumu hilo kuonekana kuwa limebebwa na jamii na jambo linaloweza kuleta taswira mbaya ndani na nje ya nchi kutokana na ukweli kuwa aliyehusika ni kiongozi na Mtanzania.

Pamoja na hayo, aliwashukuru watu wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine wakiwamo madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Dodoma kutoa huduma kwa Lissu.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )